Na Emma Kigombe
Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Tanga, Mwalimu Joseph Shayo, amewataka wanamichezo wote walioshiriki mashindano ya UMITASHUMTA ngazi ya mkoa kuendelea kudumisha nidhamu na kuongeza juhudi katika mazoezi ili kujiimarisha zaidi.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa mashindano hayo ya mkoa, Mwalimu Shayo alisema ni muhimu kwa wanamichezo hao kuendelea kufanya mazoezi kwa bidii ili waweze kuwa katika kiwango bora kitakachowawezesha kufanya vizuri zaidi katika mashindano yajayo.
Alieleza kuwa kambi ya maandalizi kwa wanamichezo waliochaguliwa inatarajiwa kuanza tarehe 25 Mei hadi 5 Juni 2026, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mashindano ya kitaifa ya UMITASHUMTA. Hata hivyo, alibainisha kuwa bado kutakuwa na mchujo zaidi katika ngazi ya mkoa ili kupata timu bora zaidi itakayoiwakilisha Tanga.
“Msibweteke, endeleeni kufanya mazoezi ya kutosha. Tunahitaji timu imara itakayoweza kushindana na kufanya vizuri katika ngazi ya taifa,” alisisitiza.
Kwa upande mwingine, Mwalimu Shayo aliwatia moyo wanamichezo ambao hawakufanikiwa kuchaguliwa kujiunga na timu ya mkoa, akiwataka kutovunjika moyo bali kuendelea kujituma. Aliwapongeza kwa kufikia hatua ya kushiriki mashindano ya ngazi ya mkoa na kueleza kuwa ushindani ulikuwa mkubwa.
Naye Afisa Michezo Mkoa wa Tanga, Digna Tesha, alisema mashindano hayo yalihusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa mikono, mpira wa kikapu, mpira wa wavu pamoja na michezo mingine, yakihusisha wavulana, wasichana na makundi maalum.
Alifafanua kuwa jumla ya wanamichezo 1,200 kutoka halmashauri zote 11 za mkoa walishiriki, ambapo kati yao wanamichezo 120 wamechaguliwa kuuwakilisha mkoa wa Tanga katika mashindano ya UMITASHUMTA kitaifa yatakayofanyika mkoani Iringa mwaka 2026.
Aidha, aliwataka wanamichezo hao watakaopata nafasi ya kuiwakilisha Tanga kujituma kwa hali ya juu ili waweze kufanya vizuri na hatimaye kupata nafasi ya kushiriki mashindano ya michezo ya shule za msingi na sekondari kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (FEASSA), yatakayofanyika mwaka huu mkoani Morogoro.
Alisisitiza kuwa mafanikio katika mashindano hayo yatategemea nidhamu, maandalizi na ushirikiano kati ya wanamichezo na walimu wao.
Mashindano ya UMITASHUMTA ngazi ya Mkoa yamebebwa na kauli mbiu isemayo “Michezo na Sanaa Shuleni, daraja la Ajira, Afya na Ushindani Kimataifa”













EmoticonEmoticon