![]() |
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia mafuta na Gesi asilia Dkt. James Mataragio amewaelekeza Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kuimarisha shughuli za utafutaji akibainisha kuwa shughuli hizo zimepungua kwa kiasi kikubwa katika miaka ya hivi karibuni
Katika Kikao chake na Menejimenti ya Mamlaka hiyo mwishoni mwa Juma hili jijini Dar es Salaam amesema moja ya maeneo yanayohitaji kipaumbele kwa hivi sasa ni utafutaji wa Gesi asilia.
Ameeleza kuwa miaka ya nyuma shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia zilikuwa zinafanyika kwa kasi kubwa, ambapo mikataba ya uzalishaji na ugawanaji wa mapato (PSA) ilikuwa zaidi ya 26, lakini kwa sasa imepungua na kufikia mikataba 11 pekee.
“Pia tukichunguza kwa kina, hata katika mikataba hiyo iliyobaki, ni kampuni chache zinazotekeleza kikamilifu majukumu yao ya kuendelea kufanya utafutaji wa mafuta na gesi asilia. Hali hii hairidhishi na inahitaji mikakati madhubuti ya kuchochea shughuli za utafutaji nchini,” alisema Dkt. Mataragio.
Aliongeza kuwa kupungua kwa shughuli za utafutaji ni hatari kwa mustakabali wa upatikanaji wa gesi asilia nchini, kwa kuwa utafutaji ndiyo hatua muhimu inayochochea ugunduzi wa rasilimali hizo na hatimaye kupelekea uzalishaji wake.
“Kwa sasa tumejipanga kama Wizara kuhakikisha tunaweka juhudi kubwa katika eneo hili pamoja na kuboresha mazingira wezeshi yatakayochochea uwekezaji na ustawi wa shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni, amesema mamlaka imeendelea kutekeleza mikakati ya kuendeleza utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini ikiwa ni pamoja na kuingia mikataba na makampuni ya kijiofizikia yaliyobobea katika ukusanyaji wa takwimu za petroli (Multi-Client Geophysical Companies) ili kuimarisha utafiti katika maeneo ya bahari kuu na nchi kavu.
Kikao hicho kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Kamishna Msaidizi wa Petroli kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Antelimi Raphael, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni, pamoja na maafisa wengine kutoka Wizara ya Nishati na PURA.









EmoticonEmoticon