RAIS SAMIA ATOA BILIONI 5.2 KUBORESHA CHUO CHA UHAMIAJI TRITA

March 15, 2026





Na Mwandishi Wetu,KILIMANJARO

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imepeleka Kiasi cha Shilingi Bilioni 5.2 kwa Idara ya Uhamiaji ili kuboresha Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda(TRITA) kilichopo Kilimanjaro ambapo Waziri Katambi ameweka wazi nia ya kuanzisha kutoa elimu katika ngazi ya Shahada,Uzamili na Uzamivu ambapo kwa sasa chuo hicho cha masuala ya uhamiaji kikitoa elimu ngazi ya Diploma.

Ametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama inayoongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo,Najma Murtaza Giga(Mb), kwa ajili ya ukaguzi wa Miradi iliyopo chini ya wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

“Ni chuo ambacho kimejikita zaidi kwenye taaluma ya soft skills(ujuzi laini) ila mafunzo ya medani yanatolewa Chuo cha Raphael Kubaga kilichopo Wilayani Mkinga,Mkoani Tanga kwa hapa tunakusudia kama tutafanya vizuri zaidi na kwa kuwa Mheshimiwa Rais anaviwezesha Vyombo vilivyopo chini ya wizara kifedha basi tuna matumaini ya kufika kwenye hatua ya kutoa elimu ngazi ya Shahada,Uzamili na Uzamivu inawezekana kwa eneo hili ukiwepo urahisi wa kufika na tunapata wanafunzi kutoka nchi za jirani” amesema Waziri Katambi

Akizungumza katika ziara hiyo Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt.Anna Makakala amesema Idara sasa inatoa mafunzo ya Kijeshi kwenye Chuo kilichopo wilayani Mkinga Mkoani Tanga ambapo hapo awali walikua wakitumia Vyuo vya Majeshi mengine kutoa mafunzo mbalimbali ya ukakamavu ikiwemo Shule ya Polisi,Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa ambapo Mkuu wa Chuo hicho cha kikanda, Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji, Hoja Mahiba akitaja wazi kutolewa kwa elimu ngazi ya Diploma sambamba na mafunzo mbalimbali kwa Maafisa Uhamiaji katika kuwajengea uwezo,kutoa mafunzo kwa wadau wanaopokea wageni wakiwemo watalii na watumishi wa serikali ikiwemo watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama,Najma Murtaza Giga(Mb) ameitaka Idara ya Uhamiaji kuweka mifumo ya teknolojia ili kusaidia maeneo mengine huku Mjumbe wa Kamati hiyo,Nape Nnauye(Mb) akishauri uanzishwaji pia wa elimu masafa ili kuweza kuwafikia wanafunzi wengi zaidi.








Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »