ONGEZEKO la idadi ya watu pamoja na kuimarika kwa shughuli za viwanda na biashara limeendelea kuchochea kasi ya mahitaji ya umeme nchini kwa wastani wa asilimia 10 hadi 15 kila mwaka.
Kutokana na mwenendo huo, Serikali imejipanga kuongeza jitihada za kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi wote, sambamba na kuimarisha miundombinu ya nishati.
Akizungumza katika mkutano wa Powering Africa Summit uliofanyika jijini Washington, DC, Machi 20, 2025, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema kuwa ongezeko hilo la mahitaji linachochea uwekezaji mkubwa katika sekta ya nishati, ambayo ni mhimili muhimu wa ukuaji wa uchumi.
Amefafanua kuwa hadi kufikia Machi 2026, uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini umefikia megawati 4,383, wakati kiwango cha juu cha mahitaji kikiwa takribani megawati 2,100.
Hata hivyo, ameonya kuwa kasi ya ongezeko la mahitaji inahitaji uwekezaji zaidi katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme ili kuendana na mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Kuhusu upatikanaji wa huduma hiyo, amesema Serikali imefanikiwa kufikisha miundombinu ya umeme katika vijiji vyote vya Tanzania Bara, ingawa kiwango cha uunganishaji wa umeme katika kaya bado ni cha chini, hali inayoonesha changamoto ya kuwafikia wananchi wote.
Mhe. Salome amesisitiza kuwa Serikali imelenga kufikia asilimia 100 ya upatikanaji wa umeme ifikapo mwaka 2030, huku ikikusudia kuongeza kiwango cha uunganishaji wa kaya hadi asilimia 75 ili kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Aidha, ameeleza kuwa Tanzania ina vyanzo mbalimbali vya nishati ikiwemo gesi asilia, maji, jua, upepo na jotoardhi, ambavyo vina uwezo mkubwa wa kukidhi mahitaji yanayoongezeka.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuhimiza matumizi ya nishati jadidifu ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa umeme, huku ikiendeleza juhudi za kuhamasisha uwekezaji katika sekta hiyo.
Hatua hizo zinatarajiwa kusaidia kukidhi mahitaji ya nishati yanayoongezeka na kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha nishati katika ukanda wa Afrika.





EmoticonEmoticon