📌*Mhandisi Mramba asema Tanzania ina fursa nyingi na mazingira ya uwekezaji ni rafiki*
New Delhi, India
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Felchesmi Mramba, ametangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika sekta ya nishati nchini, akizialika kampuni na wawekezaji wa kimataifa kuchangamkia nafasi hizo ili kuchochea ukuaji wa sekta hiyo.
Akizungumza katika kikao maalum cha India–Africa Partnership kilichofanyika wakati wa mkutano wa Bharat Electricity 2026 unaoendelea nchini India, Mhandisi Mramba amesema Tanzania ina mazingira rafiki ya uwekezaji na inaendelea kujipambanua kama moja ya maeneo yenye fursa kubwa katika sekta ya nishati barani Afrika.
Ameeleza kuwa fursa hizo zinapatikana katika maeneo mbalimbali ikiwemo miradi ya kuzalisha umeme, kusafirisha na kusambaza umeme, pamoja na uwekezaji katika nishati jadidifu kama jua, upepo, jotoardhi na umeme wa maji. Aidha, ametaja pia uwekezaji katika nishati safi ya kupikia kuwa ni eneo muhimu linalopewa kipaumbele na Serikali.
![]() |
Mhandisi Mramba ameeleza kuwa Tanzania inaendelea kukuza sekta ya umeme ili kukidhi ongezeko la mahitaji linalochochewa na ukuaji wa viwanda na ongezeko la matumizi ya umeme mijini na vijijini, akibainisha kuwa uwezo wa uzalishaji umefikia takribani megawati 4,500 na unatarajiwa kufikia megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia Mpango wa Taifa wa Nishati ( National Energy Compact) inalenga kuongeza upatikanaji wa umeme, kuimarisha matumizi ya nishati jadidifu na kufikia matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa asilimia 75 ifikapo mwaka 2030 hatua inayofungua zaidi fursa kwa wawekezaji kushiriki katika miradi yenye tija.
Amesisitiza kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na wadau wa kimataifa katika kuendeleza miradi ya kimkakati kupitia ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), akiwahakikishia wawekezaji uwepo wa mazingira wezeshi, sera thabiti na dhamira ya dhati ya Serikali katika kusimamia na kutekeleza miradi ya nishati.


EmoticonEmoticon