TAASIS
📌 *Mtambo wa gesi wazinduliwa Shule ya Azania*
Na Mwandishi Wetu
Wizara ya Nishati imesema hadi sasa taasisi 1,136 kati ya zaidi ya taasisi 30,000 zinazolisha watu zaidi ya 100 nchini zimehamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia, huku wadau wakihimizwa kuendelea kuunga mkono jitihada hizo ili kufikia lengo la kitaifa la kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.
Hayo yamesemwa leo Februari 3, 2026 na Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia, Nolasco Mlay, wakati wa uzinduzi wa mtambo wa gesi ya kupikia (LPG Vaporizer) katika Shule ya Sekondari Azania jijini Dar es Salaam.
Mtambo huo umejengwa kwa ushirikiano kati ya KAGLA Eco Friendly na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi katika taasisi za umma.
Mlay amesema nishati safi ya kupikia ni ajenda ya kimkakati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni kinara wa mpango huo nchini na barani Afrika kwa ujumla.
Amesema uzinduzi wa mtambo huo unaongeza idadi ya taasisi zinazotumia nishati safi, lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanywa kutokana na mahitaji yaliyopo.
“Kati ya taasisi zaidi ya 30,000 zinazolisha watu zaidi ya 100 nchini, ni taasisi 1,136 pekee ndizo zilizohamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia. Hivyo, bado tunahitaji ushiriki mkubwa wa wadau ili kufikia lengo la kitaifa la kuachana na mkaa na kuni,” amesema.
Ameongeza kuwa mchango wa wadau kama KAGLA Eco Friendly ni muhimu katika kufanikisha azma ya serikali ya kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Azania, Melsius Kayombo, amesema shule hiyo ina wanafunzi zaidi ya 300 na mradi wa gesi utarahisisha upishi na kuboresha ratiba za masomo.
“Tumekuwa tukiusubiri mradi huu tangu mwaka 2024. Kukamilika kwake kutapunguza muda wa maandalizi ya chakula, kulinda afya za wapishi na kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula kwa wakati ili kuendelea na masomo yao,” amesema.
Naye, Mtaalamu kutoka KAGLA Eco Friendly na mfadhili wa mradi huo, Hiroyuki Shimada, amesema teknolojia ya LPG Vaporizer iliyowekwa shuleni hapo ni salama na ya kipekee, ikiwa ni ya kwanza kutumika nchini.
Amesema mfumo huo wa kisasa una uwezo wa kutoa taarifa mbalimbali kuhusu ufanisi na usalama wa mtambo, hatua itakayosaidia taasisi kupunguza gharama za matumizi ya nishati ya kupikia.
&&&







EmoticonEmoticon