NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Chuo Kikuu cha Mzumbe, Kampasi ya Dar es Salaam, kimefungua rasmi mafunzo ya kujenga uwezo kwa taasisi mbalimbali za serikali zinazotekeleza miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia, yakilenga kuboresha mchakato wa ununuzi katika miradi ya maendeleo.
Mafunzo hayo ni sehemu ya makubaliano yaliyosainiwa kati ya Chuo Kikuu cha Mzumbe, Wizara ya Fedha na Benki ya Dunia, yakiwa na lengo kuu la kuongeza ufanisi, uwazi na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
Akizungumza leo Februari 2, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa William Mwegoha, amesema mafunzo hayo yatadumu kwa muda wa wiki mbili na yatawahusisha wataalamu kutoka sekta ya serikali na taasisi za umma wanaoshiriki katika utekelezaji wa miradi ya Benki ya Dunia.
Profesa Mwegoha amesema ni muhimu kuwajengea uwezo wataalamu wa ununuzi ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi, kwa wakati, na kwa kuzingatia sheria na taratibu za ununuzi.
“Kwa niaba ya Chuo Kikuu cha Mzumbe, tunajivunia kuwa sehemu ya ushirikiano huu. Tumejizatiti kuhakikisha tunaboresha uwezo wa taasisi za serikali ili ziweze kutekeleza miradi ya Benki ya Dunia kwa ufanisi. Kupitia mafunzo haya, tunategemea kuona miradi ikitekelezwa kwa haraka, kwa ubora, na kwa kuleta matokeo chanya kwa wananchi,” amesema Profesa Mwegoha.
Ameongeza kuwa Benki ya Dunia inatekeleza miradi mingi nchini, hali inayolazimu mchakato wa ununuzi kusimamiwa kwa njia bora na ya haraka ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa manufaa ya wananchi.
Ameeleza pia kuwa kwa mujibu wa tathmini za wataalamu, mchakato wa ununuzi umekuwa ukichukua muda mrefu, jambo ambalo limekuwa changamoto kubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mageuzi katika Sekta ya Ununuzi
Profesa Mwegoha amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mabadiliko makubwa katika sekta ya ununuzi, ambapo matumizi ya teknolojia na mifumo ya kisasa yanatarajiwa kufupisha muda wa utekelezaji wa miradi, kuongeza uwazi na kuboresha uwajibikaji.
Kwa upande wake, Kamishina Msaidizi wa Sera za Ununuzi wa Umma kutoka Wizara ya Fedha, Emma Komba, amesema mafunzo hayo yataongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Amesema Serikali, kupitia Wizara ya Fedha, ilikubaliana na Benki ya Dunia kupendekeza Chuo Kikuu cha Mzumbe kutokana na uwezo wake na uzoefu mkubwa katika utoaji wa mafunzo yanayohusu ununuzi na mnyororo wa ugavi.
“Wizara ya Fedha ilipendekeza Chuo Kikuu cha Mzumbe kwa kuzingatia uwezo wake katika kutoa mafunzo haya. Hatua iliyofikiwa leo ni matokeo ya makubaliano hayo, na sasa mafunzo yameanza rasmi kwa muda wa wiki mbili,” amesema Komba.
Naye Meneja wa Operesheni wa Benki ya Dunia kwa Tanzania, Zambia, Malawi na Zimbabwe, Milena Stenova, amesema mafunzo hayo ni hatua muhimu katika kuboresha mchakato wa ununuzi na kuchagiza utekelezaji wa miradi kwa ufanisi, huku akiwatakia washiriki mafanikio katika utekelezaji wa mpango huo.
EmoticonEmoticon