EWURA YAPONGEZWA KWA KUDUMISHA UHIMILIVU WA BEI ZA NISHATI

February 13, 2026


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kwa juhudi zake za kudumisha uhimilivu wa bei za nishati, hususan mafuta na umeme.

Amesema kuwa hatua hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kulinda maslahi ya watumiaji na kuimarisha utulivu wa sekta ya nishati nchini.

Pongezi hizo amezitoa  leo,  tarehe 13 Februari 2026, Bungeni jijini Dodoma wakati wa mafunzo  yaliyoendeshwa  na EWURA kwa Kamati hiyo, kuhusu  masuala ya ulinzi wa mtumiaji pamoja na upangaji wa bei za umeme.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe.Salome Makamba, amesema Tanzania inaendelea kuwa miongoni mwa nchi zenye bei ya chini ya umeme ikilinganishwa na mataifa mengine ya Afrika Mashariki, jambo linalodhihirisha uwepo wa mifumo madhubuti ya udhibiti na usimamizi wa sekta ya nishati.

Ameongeza kuwa udhibiti bora wa sekta ndogo ya umeme umewezesha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuboresha utendaji wake na hivyo kufanya biashara ya umeme kwa faida ikilinganishwa na ilivyokuwa awali.

Ameeleza kuwa kwa mwaka 2024/2025 TANESCO ilipata faida hadi ya takriban shilingi bilioni 545 tofauti na miaka ya nyuma ambapo kiwango cha faida kilikuwa chini ya hapo.


Naye Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi kutoka EWURA,  Bw. Msafiri Mtepa, amesema Taasisi hiyo itaendelea kuhakikisha kuwa maslahi ya Serikali, walaji na watoa huduma yanazingatiwa wakati wote ili kuwezesha upatikanaji wa huduma bora za nishati kwa gharama nafuu.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »