TRIL.1.5 ZA UMEME VITONGOJINI -WAZIRI NDEJEMBI AWASIHI MA-RC NA MA -DC KUSIMAMIA KWA UFANISHI MRADI

January 22, 2026



📌*Asema utekelezaji wa agizo la Rais Samia la kufikisha umeme katika Shule, Zahanati na Vituo vya Afya lizingatiwe*


Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amewataka viongozi na watendaji wa ngazi za Mikoa na Wilaya kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Nishati katika kusimamia utekelezaji wa Mradi wa Upelekaji Umeme katika vitongoji 9,009 nchini, ili kuhakikisha unatekelezwa kwa ufanisi na kuwanufaisha wananchi.

Mhe. Ndejembi ametoa kauli hiyo Januari 22, 2026 jijini Dodoma wakati wa Mkutano Maalum wa Tathmini ya Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa mwaka wa fedha 2024/2025, uliohudhuriwa na Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Waganga Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Maafisa Lishe wa Mikoa.

Amesema mradi huo unagharimu zaidi ya Sh.trilioni 1.5, fedha zinazotokana na walipa kodi wa Tanzania, hivyo kuna wajibu wa pamoja wa kuhakikisha zinatekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia thamani ya fedha.


“Mradi huu unatekelezwa kwa fedha za Watanzania, hivyo tuna wajibu mkubwa wa kuusimamia kikamilifu. Mafanikio yake yanategemea ushirikiano wenu kama waratibu wa sekta zote katika maeneo mnayoyasimamia,” amesema Ndejembi.

Aidha, amewakumbusha viongozi hao kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, la kuhakikisha shule zote, vituo vya afya na zahanati zinafikishiwa umeme kupitia mradi huo, hata kama zipo nje ya umbali wa mita 30 kutoka kwenye miundombinu ya mradi.


Kuhusu gharama za kuunganisha umeme vijijini, Waziri Ndejembi amefafanua kuwa ni sh.27,000 kwa wananchi waliopo ndani ya mita 30 ya mradi, wakati wa utekelezaji na hadi ndani ya miezi mitatu baada ya kukamilika kwa mradi. 



Kutokana na hilo, amewataka viongozi wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri kuwahamasisha wananchi kutumia fursa hiyo mapema.


Hata hivyo, ili kuharakisha uunganishaji wa umeme, Waziri Ndejembi ameelekeza kuwa hata  wananchi ambao hawajakamilisha utandazaji wa nyaya katika nyumba zao (partial wiring) waingiziwe umeme bila kusubiri ukamilishaji wa nyumba nzima.


Katika hatua nyingine, amewasisitiza viongozi hao kuzindua miradi ya umeme mara inapokamilika katika maeneo yao bila kusubiri viongozi wa Wizara ya Nishati kufika, ili wananchi waanze kunufaika haraka.


Amesema Wizara ya Nishati inaweka utaratibu madhubuti wa ufuatiliaji wa miradi ya umeme kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Wilaya, ili kuhakikisha utekelezaji unakuwa wa ufanisi na kwa viwango vinavyokubalika.


Pamoja na hayo, amewataka viongozi hao kusaidia kurahisisha upatikanaji wa vibali vya ujenzi wa miradi ya umeme katika maeneo ya misitu, kuhakikisha wakandarasi wanakuwepo kwenye maeneo ya kazi, pamoja na kuwaelimisha wananchi kushirikiana na wakandarasi bila vikwazo na kwamba miradi ya umeme vijijini haina fidia.


Akitoa takwimu za mradi wa umeme vitongojini, Mhe. Ndejembi amesema kuwa kati ya vitongoji takribani 64,400 vilivyopo nchini, vitongoji 23,000 vilikuwa bado havijafikiwa na umeme. Kupitia utekelezaji wa mradi wa sasa wa kupeleka umeme katika vitongoji 9,009, vitongoji vitakavyobaki bila umeme vitapungua hadi takribani 13,413 pekee nchi nzima.


Mgeni rasmi katika mkutano huo alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe.


&&&&

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »