Na Oscar Assenga,TANGA
SERIKALI Mkoani Tanga imetangaza kuanzisha Jukwaa Vijana la Mkoa litakalosaidia vijana kuelewa na kutumia mifumo ya kidijitali ya upatikanaji wa mikopo inayotolewa kupitia mamlaka za serikali za mitaa.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi, Dkt Batilda Burian katika kikao maalumu kilichowakutanisha viongozi wa dini, wawakilishi wa wanafunzi kutoka vyuo vya ndani ya jiji na viongozi wa makundi ya kijamii
Alisema kwamba atawaelekeza maafisa Maafisa Maendeleo ya Jamii kuwafuata vijana walipo na kuwapatia mwongozo sahihi kuhusu uundaji wa vikundi vya kiuchumi vinavyoweza kupata mikopo hiyo.
“Katika suala hili tutaanzisha jukwaa la vijana mkoa litakalokuwa na lengo la kuwasaidia kuelewa namna ya kutumia mifumo ya kidigitali ya upatikanaji wa mikopo inayotolewa kupitia Halmashauri kwa lengo la kuweza kujikwamua kiuchumi”Alisema
Katika hatua nyengine ,Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda alitoa wito kwa vijana wa Tanga na Tanzania kwa ujumla kutumia mitandao ya kijamii kwa umakini na kunufaika na fursa zinazoletwa na majukwaa hayo badala ya kuvutwa na mitindo ya mtandaoni yenye upotoshaji inayowafanya wawe rahisi kudhibitiwa na kuchochewa kuingia kwenye vurugu zinazoendeshwa na mataifa ya kigeni.
Mkuu huyo wa mkoa alionya kuwa gharama ya kupoteza amani huwaathiri zaidi vijana kutokana na pale inapopotea vijana wanaumia zaidi hivyo wajiepushe na vitendo vya namna hiyo.
“Pale amani inapopotea vijana wanaoumia zaidi na hata Uharibifu wa miundombinu na kusimama kwa programu za kiuchumi huleta madhara ya muda mrefu yanayogusa moja kwa moja mustakabali wao.”Alisema
Alisema kwamba Tanzania imejaliwa rasilimali nyingi za asili jambo linaloifanya kuwa shabaha ya mataifa yanayotafuta ushawishi na upatikanaji wa rasilimali hizo.
Alionya kuwa pale baadhi ya mataifa yanaposhindwa kupata mikataba halali ya uwekezaji, huishia kutumia mbinu za kificho ikiwemo kutumia mitandao ya kijamii na mawakala wanaolipwa kuchochea hali ya sintofahamu ili baadaye warejee kama wapatanishi na kuibuka na mikataba ya unyonyaji.
“Tumeona mbinu kama hizo maeneo mengine, kama Goma,” alisema. “Nchi inayojulikana kwa kuchochea vurugu hujitokeza baadaye kama mpatanishi lakini ndiye mnufaika mkubwa wa machafuko na mikataba inayofuata.”
Aliongeza kuwa hali ya Sudan pia inaonyesha jinsi mataifa tajiri yanavyoweza kuwa wahanga wa njama za kisiasa za kimataifa.
Mkuu huyo wa mkoa alisisitiza kuwa serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika mkoa wa Tanga katika miundombinu, viwanda na programu za kijamii na kwamba uwekezaji zaidi unaendelea.
Aidha, Dkt. Burian alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatekeleza ahadi zake za siku 100, ikiwemo kupanua fursa za kiuchumi, kuvutia uwekezaji mpya, kuongeza ajira, kupanua upatikanaji wa mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri, na kuendeleza mipango ya bima ya afya kwa wote.
Akizunhumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa Wajasiriamali wa Soko la Tangamano Esin Mohamed alisema vijana wengine hujikuta wakitumiwa kwa sababu hawana majukwaa ya kueleza changamoto zao.
“Viongozi na maafisa wa serikali wanapaswa kushuka walipo vijana na kusikiliza maoni yao,” alihimiza.
Mshiriki mwingine, Mussa Mbaruk, Mwenyekiti wa CUF Mkoa wa Tanga, alisema wadau wanapaswa kukabiliana na mizizi ya misuguano badala ya kukwepa mijadala migumu.
“Ni lazima tuanze kwa kutoa haki katika maeneo yote,” alisema.
EmoticonEmoticon