📌 *Mashine ya kutengeneza mkaa mbadala kutolewa kuongeza nguvu ya uzalishaji nishati salama*
📌 *Ni hatua ya Serikali kuimarisha utekelezaji wa matumizi ya nishati safi katika taasisi*
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) italipelekea Gereza la Kasulu mkoani Kigoma mashine moja ya kisasa ya kutengeneza mkaa mbadala, hatua inayolenga kuliwezesha gereza hilo kuondokana na njia duni zilizokuwa zikitumika awali kuzalisha mkaa mbadala.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika gereza hilo, Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Bw. Nolasco Mlay, amesema Serikali inaendelea kuunga mkono jitihada za taasisi mbalimbali nchini katika kuachana na nishati zisizo salama kwa kuwezesha upatikanaji wa teknolojia rafiki kwa mazingira.
Amesema utoaji wa mashine hiyo utapunguza changamoto za upatikanaji wa mkaa mbadala kutoka maeneo ya mbali, kupunguza gharama za uendeshaji pamoja na kuimarisha uzalishaji wa nishati safi kwa kutumia malighafi zinazopatikana kwa urahisi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza la Kasulu, Bw. Vitalis Mkali, ameishukuru Serikali kwa hatua hiyo akisema mashine hiyo itasaidia kuzalisha mkaa mbadala wa kutosha, kuachana na mbinu duni za awali na kupunguza gharama zilizokuwa zikijitokeza wakati wa ununuzi wa nishati.
Amesema hatua hiyo itaongeza ufanisi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ndani ya gereza sambamba na kulinda mazingira na kuboresha afya kwa watumiaji wa nishati hiyo.
Ziara ya Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia katika magereza mbalimbali ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Serikali la kuhakikisha taasisi zote zinazohudumia zaidi ya watu 100 nchini zinatumia nishati safi ya kupikia kama mkakati wa kulinda mazingira, kupunguza ukataji miti na kuboresha ustawi wa jamii.








EmoticonEmoticon