MKURUGENZI MKUU REA AWAFUNDA WATUMISHI

December 16, 2025


📌Awasisitiza kufanya kazi kwa Bidii, Uadilifu na Maarifa


📌Asisitiza ushirikiano na kufanya kazi kwa pamoja


📌Awasisitiza, kuheshimiana, kupendana na kutimiza wajibu wao


📍Dodoma


Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amewataka watumishi kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na maarifa ili kuleta tija katika kuwatumikia wananchi.


Ametoa rai hiyo Jijini Dodoma Desemba 15, 2025 katika kikao kazi na watumishi wote wa Wakala.

"Mnafanya kazi nzuri, ndani ya miaka mitano kazi kubwa imefanyika lakini hatupaswi kubweteka, wananchi waishio maeneo ya vijijini wanatutegemea kwenye suala la Nishati, hatupaswi kuwaangusha," alisisitiza Mhandisi Saidy.

Mhandisi Saidy alisema kuwa kila Kitengo na Idara ndani ya Wakala kina jukumu na wajibu wa kufanya ili kutimiza dhamira ya Serikali la kuwasambazia wananchi wake Nishati bora na aliwaasa watumishi wote kufanya kazi kwa kushirikiana bila kutazama Idara ama Kitengo anachotoka.

"Tufanye kazi, sisi ni timu moja; tuepuke kuwa chanzo cha migogoro; kama kuna jambo linakutatiza zungumza na watumishi wenzako, nenda kwa wahusika ili upate ufumbuzi na tusiruhusu majungu maeneo yetu ya kazi," alisisitiza Mha. Saidy.


Alisisitiza kuwa umeme sio jambo la anasa bali ni kichocheo muhimu cha maendeleo na kwamba wananchi waishio vijijini wanayo matarajio makubwa ya kuunganishiwa umeme.

Akizungumzia baadhi ya mafanikio, Mhandisi Saidy alisema hadi sasa vijiii vyote nchini vimefikishiwa umeme na kwamba kazi ya kusambaza umeme vitongojini inakwenda kwa kasi na matarajio ni kufikisha lengo lililowekwa hata kabla ya muda.


"Ilani ya CCM inasema, Serikali ikamilishe zoezi la kupeleka umeme katika vitongoji 31,000 vilivyobaki ifikapo 2030. Hadi sasa vitongoji 17,500 vishafikishiwa huduma na vishaingizwa katika miradi au mipango ya kupatiwa umeme hivyo vimebaki vitongoji 13,500 tu. 


Mha. Saidy alisisitisa kuwa, wao kama Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inawajibu wa kuhakikisha kuwa vitongoji vilivyobaki 13,500 navyo vinapatiwa umeme kabla ya 2030.


Vilevile aliwasisitiza watumishi kujenga tabia ya kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao na hivyo kuleta tija katika utendaji wao wa kila siku.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala REA, Renatus Msangira aliwakumbusha watumishi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na taratibu za utumishi wa umma.


Mwisho

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »