MHE.MCHENGERWA ATUA ALGERIA, AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA MKUTANO WA UZALISHAJI WA DAWA NA TEKNOLOJIA AFRIKA.

November 26, 2025

Na Mwandishi Wetu, Algiers

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa leo amewasili nchini Algeria akiwa ameongoza ujumbe kutoka nchini Tanzania kuja kushiriki Mkutano wa Mawaziri kuhusu Uzalishaji wa Ndani wa Dawa na Teknolojia barani Afrika unaotarajia kuanza hapo kesho.

Mheshimiwa Mchengerwa na ujumbe wake umepokewa na Balozi wa Tanzania nchini Algeria Mhe. Iman Njalikai na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Kanda ya Afrika, Prof. Mohamed Janabi tayari kwa ajili ya mkutano wa kesho.

Mkutano huo pamoja na mambo mengine unalenga kuimarisha sekta ya dawa na teknolojia ya afya barani Afrika kama ilivyoazimiwa wakati wa kikao cha 74 cha Shirika la Afya Duniani - Kanda ya Afrika kilichofanyika Agosti 2024.

Katika Mkutano huo nchi mbalimbali zimealikwa ikiwa ni pamoja na Uganda, Zimbabwe, Jamhuri ya Kongo, Niger, Chad, Jamhuri ya Kudemokrasia ya Kongo na Madagascar.
Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi zilizopewa kipaumbele cha kushiriki mkutano huo kutokana na kuthamini uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu na kihistoria wa nchi hizo mbili toka enzi za Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.

Aidha, mkutano huu ni fursa ya kipekee kwa Tanzania kuweza kunufaika kwa kujenga ushawishi ili kupata fursa ya kutumia utaalamu, teknolojia kutoka kwa wazalishaji wa dawa wa Algeria ambao wamepiga hatua kubwa katika sekta hiyo barani Afrika.
Ikumbukwe pia kuwa kuimarisha uzalishaji wa ndani wa dawa barani Afrika ilikuwa mojawapo ya ajenda mahususi ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika Prof.Janabi wakati akigombea nafasi hiyo.


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »