TANESCO YAPATA TUZO YA UTOAJI HUDUMA BORA KWA WATEJA 2025

October 11, 2025


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.


📌*Yatajwa kama Taasisi pekee ya umma kushinda katika tuzo hizo*


📌*Yadhihirisha kufanikiwa kwa mikakati ya kuboresha huduma kwa wateja*


Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeibuka mshindi wa kwanza wa Tuzo ya Utoaji Bora wa Huduma kwa Wateja kwa mwaka 2025 kwa taasisi za Serikali zinazotoa huduma ya nishati katika tukio la tuzo hizo zilizofanyika katika wiki ya huduma kwa wateja iliyoanza tarehe 6 – 10 Oktoba 2025.


Tuzo hizo zilizofanyika katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam na kuzikutanisha taasisi na kampuni mbalimbali kutoka sekta za umma na binafsi zenye zinazotoa huduma mbalimbali nchini Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah ambae pia ndie aliyekuwa mgeni rasmi alizipongeza taasisi zote zilizoshiriki na kuonyesha ubunifu katika utoaji huduma, huku akisisitiza kuwa taasisi za umma zina wajibu mkubwa wa kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa wananchi kwa wakati na kwa viwango vinavyokidhi matarajio ya wateja. 


“Niwapongeze wenzetu ambao wamepata hizi tuzo na wale walioandaa kwa sababu tunapowapa hizi tuzo inawasaidia kuwaonyesha kile wanachokifanya kinafuatiliwa kwa karibu. Taasisi zote ambazo zimepata tunazifahamu na tunaeelewa umuhimu mkubwa kwa kila wanachokifanya. Kwa wale ambao hawajapata nao wameona ipo namna ya kwenda kuboresha huduma zao,” alisema Dkt. Abdallah.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja, Bi. Irene Gowelle, licha ya kuwashukuru waandaaji wa tuzo hizo alisema tuzo hiyo ni kielelezo cha mikakati na kazi kubwa ambayo shirika limefanya katika kuboresha namna ya kuwahudumia wateja.


“Tuzo hii iende kuchochera ari na mwamko wa kuendeleae kufanya kazi kwa bidii ya kuendelea kuwahudumia watanzania na kuhakikisha kuwa tunaendelea kushinda tuzo nyingine. Hakika tunajivunia kuwa taasisi ya umme pekee iliyofanikiwa kushinda tuzo katika huduma kwa wateja 2025,” aliongeza Bi. Gowelle.


Aidha Bi. Gowelle ametoa shukrani kwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa inayoufanya kwa TANESCO kupitia Wizara ya Nishati  jambo linalopelekea upatikanaji wa uhakika wa huduma ya umeme nchini.


Tuzo  zimeandaliwa na Kamati ya Kitaifa ya Wiki ya Huduma kwa Wateja chini ya uratibu wa kampuni ya uandaaji wa matukio ya wiki ya huduma kwa wateja ya CSW Tanzania Events zikiwa na lengo la kutambua na kupongeza taasisi na kampuni zinazofanya kazi nzuri katika eneo la huduma kwa wateja.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »