📍Jumla ya megawati 70 zaongezeka katika mikoa ya Lindi na Mtwara
📍RC Mtwara kuuzindua Mtambo huo tarehe 27/10/2025
Na Charles Kombe, Mtwara.
Kazi ya ufungwaji wa Mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia katika Kituo cha TANESCO cha Mtwara II umekamilika kwa ufanisi mkubwa, na tayari mashine mpya imeanza kufanyiwa majaribio ya kuanza kuwahudumia wakazi wa mikoa ya Kusini mwa Tanzania ya Mtwara na Lindi.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya kazi ya ufungwaji wa mtambo huo, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja, Bi. Irene Gowelle, amesema hatua hiyo ni ushahidi wa utekelezaji wa mipango ya serikali ya awamu ya sita ya kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini.
“Kwa mafanikio makubwa, ile kazi ya ufungaji wa mashine ya kuzalisha umeme kwa njia ya gesi asilia ambayo imekuwa ikiendelea katika kituo chetu cha Mtwara II, imekamilika kwa ufanisi mkubwa na kabla ya muda ambao tuliutangaza na hivi sasa uanfanyiwa majaribio kwa ajili ya kuangalia ufanisi na namna itaendelea kuwahudumia wateja wetu,” amesema Bi. Gowelle.
Ameongeza kuwa mashine hiyo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe Kanali Patrick Sewala hivi karibuni, na itakuwa ni nyongeza muhimu kwa nguvu ya uzalishaji wa umeme katika mikoa ya Mtwara na Lindi.
“Hizi zote ni jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anapata huduma ya umeme wa uhakika,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Uzalishaji Umeme TANESCO, Mhandisi Antony Mbushi, amesema kukamilika kwa mradi huo kunamaanisha ongezeko la uzalishaji wa megawati 20 zaidi kwa kanda ya kusini.
“Awali tulikuwa na uwezo wa megawati 50.5, lakini sasa tutakuwa na jumla ya megawati 70 katika mikoa yetu ya Mtwara na Lindi. Tunaendelea kuwahakikishia wateja wetu kuwa umeme upo wa kutosha na wa uhakika,” amesema Mha. Mbushi.
Naye mtaalamu wa umeme, Bw. Fikiri Khalifa, amesema kazi hiyo imekamilika kwa kasi isiyotarajiwa.
“Tulitarajia mwisho wa mwezi ndio mashine ingeanza kazi, lakini tumekamilisha kabla ya muda huo. Hili ni jambo kubwa katika utekelezaji wa miradi ya kitaifa,” amesema Bw. Khalifa.
Kufungwa kwa mtambo huu ni sehemu ya juhudi za serikali kuongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa Watanzania wote, hasa katika maeneo ambayo yamekuwa yakikumbwa na changamoto za upungufu wa umeme kwa miaka mingi ya Mtwara na Lindi.
EmoticonEmoticon