📌Aipongeza TANESCO kwa mpango wa ukopeshaji wa majiko wateja
wanaounganishiwa umeme
📌Asema ni wazo la kibunifu kuongeza wateja wa umeme na watumiaji wa umeme kupikia
Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Albert Chalamila amezindua program ya Konekt Umeme Pika kwa Umeme ukiwa ni utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Nishati (Energy Compact), wenye lengo la kuunganisha wateja milioni 8.5 ifikapo mwaka 2030, sawa na takribani wateja milioni 1.7 wapya kila mwaka.
Akizungumza katika uzinduzi huo Oktoba 09.2025 katika viwanja vya Mwembeyanga Jijini Dar es salaam Mhe Mhe. Chalamila ameipongeza ,Wizara ya Nishati, TANESCO na wadau wote wa maendeleo kwa kuja na wazo hili bunifu lenye lengo la kuongeza idadi ya wateja wanaounganishiwa umeme pamoja na upatikanaji wa nishati safi ya kupikia.
Pamoja na hayo Mhe. Chalamila amesema mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa yakichangia changamoto ya ukame hivyo ameitaka jamii kuwa mstari wa mbele kuhakikisha inalinda mazingira na kutunza miundombinu ya umeme.
‘’Niwapongeze sana TANESCO kwa kuja na mpango huu, hakika mmeibeba ajenda ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na ninafurahi sana kwa jiji la Dar es salaam umeme umefika kila sehemu na tumeshuhudia maboresho ya miundombinu ya umeme. Ninaamini kwa jitihada hizi wananchi wengi watahamasika kutumia umeme kupikia,’’alisisitiza Mhe. Chalamila.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. Lazaro Twange amefafanua kuwa mpango huu ni mwanzo wa zama mpya katika historia ya huduma za umeme nchini ambapo kwa hatua ya kuwaunganishia wateja wapya na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya umeme kupikia kunaifanya jamii ya Kitanzania kuwa katika viwango bora vya maisha.
‘’Tumeamua kusogeza huduma zetu karibu na wateja, kwetu mteja ni zaidi ya neno lenyewe tumekuwa tukifanya jitihada za makusudi katika kumuhudumia na kupitia ushirikiano na MECS, TANESCO imeandaa mpango wa kuhakikisha kila mteja mpya anae unganishiwa umeme anapata jiko la umeme sanifu mara tu baada ya kufungiwa huduma ya umeme, ‘’,
ameeleza Twange.
Naye Mwakilishi wa Mpango wa MECS ulio chini ya Serikali ya Uingereza Bw. Charles Barnabas ambao ndio wanadhamini wa mpango wa huduma za kisasa za kupikia (MECS) amesema kwa kushirikiana na TANESCO mpango huu utachagiza ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme kwa wananchi.
Hafla ya uzinduzi huu umeenda sambamba na kauli mbiu isemayo Konekti umeme, pika kwa umeme ambapo wateja ambao wameunganishiwa umeme walikopeshwa majiko yanayotumia umeme kidogo kupikia na kukabidhiwa na Mgeni rasmi ambayo watayalipa kwa kipindi cha miezi sita hadi mwaka mmoja kupitia manunuzi ya umeme.
EmoticonEmoticon