-AWAOMBA WATANZANIA KUPIGA KURA ZA KUTOSHA KWA CCM
Na Mgeni Reuben
Mgombea wa Jimbo la Rufiji Mohamed Mchengerwa amesema kwa sasa kila mtanzania anajua kazi kubwa iliyofanywa na CCM kubadilisha maisha ya watanzania, na kuwaomba ifikapo Oktoba 29, mwaka huu kumchagua mgombea wa Urais, Mhe. Samia Suluhu Hassan ili aendeleze pale alipoishia.
Mchengerwa amesema hayo jana wakati wa mkutano wa hadhara wa Mgombea Mwenza wa kiti cha urais kupitia CCM, Mhe. Dkt Emmanuel Nchimbi uliofanyika Nyamwage jimboni Rufiji.
Mhe. Nchimbi alimwombea kura Mchengerwa huku akisisitiza kuwa Mhe. Mchengerwa ni miongoni mwa wasaidizi wa Rais ambao wamefanya kazi nzuri katika nyazifa mbalimbali Serikalini katika kipindi chote.
Akitoa hotuba yake huku akishangiliwa na mamia ya wananchi wa Rufiji, Mhe. Mchengerwa amesema Rais Samia ni Rais wa kipekee ambaye ameweza kuendeleza miradi yote ya mtangulizi wake hayati Rais Magufuli na kutimiza ndoto za baba wa taifa Mwalimu Nyerere kwa mafanikio makubwa.
Amewaomba wananchi kukipigia kura nyingi za heshima CCM kuanzia ngazi ya urais, ubunge na udiwani huku akifafanua kwa kina maendeleo lukuki yaliyofanyika katika kipindi hiki kwenye Jimbo la Rufiji.
Ameyataja baadhi ya mafanikio kuwa ni pamoja na kufikisha umeme katika vijiji vyote 38 toka vijiji 5 tu vya awali, kuongezeka kwa shule za Sekondari 24 toka 4 pia vituo vya afya 3 hadi 9 na kuwa na mtandao wa barabara wa zaidi ya kilometa 20 ambapo awali hakukuwa na hata barabara hizo.
Ametumia fursa hiyo kuomba Serikali kuongeza fedha katika eneo la kilimo kwa kuwa ardhi ya jimbo hilo ina rutuba ya kutosha kwa ajili mazao mbalimbali.
Aidha, ameomba uwezekano wa kupatiwa Mkoa kwa kuwa hivi sasa baadhi ya maeneo ni zaidi ya kilometa 400 kufikia Ofisi ya Mkoa.
Kwa upande wa Nchimbi amewaahidi wananchi wa Jimbo la Rufiji endapo CCM kitapata ridhaa watakwenda kuboresha hospitali ya Wilaya hiyo, kujenga zahanati tano, vituo vya afya vinne na kuongeza nyumba saba za walimu.
Pia shule nne za msingi na madarasa 214 kwenye shule za zamani.
Aidha, amefafanua kuwa katika sekta ya kilimo licha ya Serikali kuongeza kiasi kikubwa cha fedha katika kipindi chote pia watajenga skimu maalum za umwagiliaji, stendi na soko la kisasa katika eneo la Ikwiriri.
EmoticonEmoticon