*📌 Ni kutokana na mabadiliko ya kidijitali katika utoaji wa huduma kwa Wateja*
*📌 Waahidi kuongeza ufanisi katika Taasisi zao kupitia mafunzo waliyoyapata*
Na. Josephine Maxime, Dar es Salaam
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limepongezwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) pamoja na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) kwa uwekezaji wake mkubwa katika teknolojia ya mawasiliano ambao umeimarisha kwa kiwango kikubwa huduma kwa wateja.
Pongezi hizo zimetolewa na viongozi wa Taasisi hizo baada ya kufanya ziara ya mafunzo katika Kituo cha Huduma kwa Wateja cha TANESCO (Call Center), aambapo walishuhudia jinsi mifumo ya TEHAMA na huduma kwa wateja zinavyoshirikiana kutatua changamoto kwa haraka na kuongeza ufanisi.
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja TANESCO, Bi. Irene Gowelle, amesema TANESCO imekuwa ikifanya jitihada kubwa kuboresha huduma kwa wateja hatua ambayo imechangiwa pia na uwekezaji uliofanyika katika teknolojia.
“Tunaona matunda ya uwekezaji huu mkubwa uliofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Nishati. Sasa taasisi nyingi zinakuja kujifunza kutoka kwetu, jambo ambalo awali halikuwepo. Lengo letu ni kuhakikisha kila mteja anapata majibu kwa haraka na changamoto zake zinatatuliwa kwa ufanisi,” alisema Bi. Gowelle.
Kwa upande wao, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa MORUWASA, Bw. Kiguhe Benno Lyang’onjo, na Afisa Habari Mkuu kutoka BRELA, Bi. Joyce Mgaya, wamesema wamevutiwa na namna TANESCO ilivyowekeza katika mifumo ya mawasiliano, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza malalamiko ya wateja na kuongeza ufanisi wa huduma.
“TANESCO mmepiga hatua kubwa katika matumizi ya teknolojia ya mawasiliano. Mafunzo haya yametupa mwanga wa namna bora ya kuimarisha huduma kwa wateja katika taasisi zetu. Tutayatumia kuleta mageuzi chanya,” alisema Bi. Mgaya.
Ziara hii ni sehemu ya utaratibu wa mashirika ya umma kushirikiana na kujifunza kutoka kwa wenzao waliopiga hatua katika maeneo mbalimbali ya kiutendaji, ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
EmoticonEmoticon