
Na Mwandishi Wetu, Handeni
HALMASHAURI ya Mji Handeni mkoani Tanga imeandika historia mpya baada ya kukamilisha ujenzi wa Shule ya Amali ya Mapinduzi, hatua itakayowaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali wa kilometa 22 kila siku kufuata elimu katika Shule ya Sekondari Kwenjugo.
Mradi huo uliofadhiliwa na serikali kupitia Mpango wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) umegharimu zaidi ya Sh. milioni 584.2 na unatajwa kuongeza ufaulu pamoja na hamasa ya wanafunzi kushiriki kikamilifu masomo yao.
Akizungumza mara baada ya kukagua shule hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni, Maryam Ukwaju, ameishukuru serikali kwa kuendelea kutoa kipaumbele katika uboreshaji wa miundombinu ya sekta ya elimu.
“Nimpongeze sana Mkuu wa Shule ya Sekondari Kwenjugo, John Rajabu, pamoja na Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari, Hadija Kingimali, kwa usimamizi mzuri hadi kukamilisha ujenzi wa shule hii. Hii ni hatua kubwa ya kuwaondolea adha watoto kutembea umbali mrefu kufuata elimu,” amesema.
Amesema kukamilika kwa shule hiyo kunatekeleza kwa vitendo dhamira ya serikali ya kuhakikisha elimu bora inapatikana karibu na jamii.
Pia ameelekeza kufanyike uthamini ili kuongeza eneo la shule hiyo kwa ajili ya viwanja vya michezo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari, Hadija Kingimali, alisema shule hiyo mpya ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 320.
“Tunatarajia shule zinapofunguliwa Septemba 15, wanafunzi 53 wa kidato cha kwanza waliokuwa wakisoma Sekondari ya Kwenjugo watahamishiwa rasmi kuendelea na masomo katika shule hii,” ameema Kingimali.
Awali, akisoma taarifa ya ujenzi, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kwenjugo, John Rajabu, amesema mradi huo ulianza Septemba 27, 2024 kwa kujengwa majengo 13 ya kisasa yakiwemo maabara za kemia na biolojia pamoja na jengo la Tehama.




EmoticonEmoticon