TANESCO YAANZA ZOEZI LA UKAGUZI WA MITA KUBAINI UPOTEVU NA WIZI WA UMEME UNAOFANYWA NA BAADHI YA WATEJA

August 08, 2025


📌Zoezi limeanza kwenye maeneo yote nchi nzima


📌Shirika laomba ushirikiano wateja wake katika kubaini wezi wa umeme ili kudhibiti mapato


📌Ofisi ya huduma kwa wateja wilaya ya kibamba yazinduliwa


Kibamba, 07 Agosti 2025

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetangaza kuanza kwa zoezi la ukaguzi wa mita za wateja nchini ili kudhibiti mapato na kubaini wateja wasio waaminifu wanaotumia umeme bila kulipia.


Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na huduma kwa wateja wa TANESCO Bi. Irene Gowelle wakati akizindua Ofisi ya Huduma kwa Wateja ya Kinondoni Kusini, iliyoko Kibamba, ikiwa ni jitihada za kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma na kusogea karibu zaidi na wananchi.

"Tumekuwa na changamoto ya upotevu wa mapato kutokana na mita zisizofanya kazi vizuri kutokana na umri lakini pia wako baadhi ya wateja ambao si waaminifu wamekua wakichezea mita kuiba umeme sasa zoezi hili litahakikisha tunazikagua mita hizo na kuchukua hatua kali za kisheria kwa wale watabainika ni wezi wa umeme" alisisitiza Gowelle


Pamoja na hayo ametoa rai kwa wananchi na wateja kutumia mfumo wa utoaji taarifa za siri uliozinduliwa hivi karibuni kuwabaini na kuwafichua wale wote wanaolihujumu shirika kwa kuiba umeme na kuwahakikishia usalama wao na ulinzi kwa watoa taarifa.

Katika hatua nyingine Gowelle, amepongeza uongozi na wafanyakazi kwa wa Mkoa wa Kinondoni kusini kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kuboresha mazingira mazuri ya ofisi hiyo.


“Uwepo wa ofisi hii mpya ni hatua muhimu katika kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi. Matatizo ya wateja sasa yatatatuliwa kwa haraka zaidi kwa kuwa tumesogeza huduma karibu nao,” alisema Bi. Gowelle.


Aidha Bi. Gowelle amesisitiza matumizi sahihi ya umeme kama nishati salama na rafiki kwa mazingira katika shughuli za kupikia, akihamasisha wananchi kuunga mkono kampeni ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kupikia kwa gharama nafuu.



Ametoa rai kwa wafanyakazi wa Ofisi hiyo kuipenda na kuitunza kwa uaminifu, sambamba na kuendelea kutoa huduma kwa ufanisi. Pia alisisitiza kuimarishwa kwa ushirikiano baina ya idara ya ufundi na idara ya huduma kwa wateja, pamoja na kuendeleza utoaji wa elimu ili kuboresha zaidi huduma kwa wananchi.


Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO Kibamba, Bi. Salma Yahya Muharam, amemshukuru Mgeni rasmi kwa kushiriki katika uzinduzi huo na ameipongeza Serikali kwa kuwezesha ujenzi wa Ofisi hiyo. Ametoa wito kwa wafanyakazi kuendelea kushirikiana ili kupunguza malalamiko ya wateja na kuhakikisha huduma bora zaidi zinatolewa.


Tayari Shirika limeanza kuwakamata na kuwachukulia hatua baadhi ya wateja wanaoiba umeme au kujiunganishia isivyo halali kwenye maeneo mbalimbali kote nchini.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »