TBS Kanda ya Mashariki Yateketeza Tani 64 za Vipodozi Vyenye Viambata sumu

July 15, 2025
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) kupitia ofisi ya Kanda ya Mashariki limekamata na kuteketeza tani 64 za vipodozi vyenye thamani ya takribani Shilingi milioni 150, baada ya kubainika kuwa bidhaa hizo zimekwisha muda wake wa matumizi na baadhi yake kuwa na viambata sumu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 15, 2025 Mkuranga mkoani Pwani, Meneja wa TBS Kanda ya Mashariki Bi. Noor Meghji, alisema kuwa ukaguzi uliopelekea kukamatwa kwa bidhaa hizo ulifanyika kati ya mwezi Januari hadi Juni 2025.

“Vipodozi hivi vimeondolewa sokoni kutokana na kuisha muda wake wa matumizi, lakini pia kuna baadhi ambavyo vimepigwa marufuku na vyenye viambata sumu ambavyo vyote havifai kwa matumizi ya binadamu,” alisema Bi. Meghji.

Aidha, Bi. Meghji alitoa wito kwa watumiaji wa bidhaa mbalimbali kuangalia maelezo ya vifungashio kabla ya manunuzi.

“Iwapo mtumiaji atagundua tofauti yoyote kwenye bidhaa au kipodozi anachokitumia, ni vyema kutoa taarifa mapema ili hatua zichukuliwe,” aliongeza.

Pamoja na hayo Bi. Meghji alibainisha kuwa TBS haikusudii kuwaumiza wafanyabiashara kwa kuharibu bidhaa zao, ndo maana inatoa elimu kila wamati na kuweka wazi orodha ya bidhaa zilizopigwa marufuku pamoja na zile zenye viambata hatarishi kupitia tovuti yao rasmi: www.tbs.go.tz.

Wakati huohuo, TBS imetoa onyo kwa wafanyabiashara wanaouza bidhaa ambazo hazijakidhi viwango vya ubora au zinazohatarisha afya ya jamii.

Shirika hilo limesema halitasita kuchukua hatua kwa watakaobainika kukiuka sheria, ikiwemo kulazimika kugharamia uteketezaji wa bidhaa na kuchukuliwa hatua zaidi za kisheria kwa waliokiuka kwa makusudi.

TBS imesisitiza dhamira yake ya kuhakikisha biashara bidhaa zote zinazoingizwa au kuzalishwa ndani ya nchi zinazingatia viwango husika kwa lengo la kulinda uchumi na afya ya umma.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »