Jumla ya makala 253 zinazohusu masuala ya uhuru wa habari Zanzibar zimeripotiwa na kuchapishwa kupitia magazeti, redio za kijamii na kitaifa pamoja na mitandao ya kijamii. Makala hizo zimeandikwa na waandishi wa habari 25 waliopata mafunzo maalum kutoka vyombo mbalimbali vya habari vya Unguja na Pemba.
Hayo yameelezwa na Afisa Programu ya Mapitio ya sheria na uhuru wa habari kutoka TAMWA-ZNZ, Zaina Abdalla Mzee, wakati akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa programu hiyo. Katika wasilisho hilo Zaina alibainisha mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza pamoja na mikakati ya baadaye kwa ajili ya kuendeleza juhudi za kulinda na kuimarisha uhuru wa habari visiwani Zanzibar.
Zaina alibainisha kuwa juhudi za ushawishi na uchechemuzi zilizofanywa na wadau wa habari, wakiwemo Wajumbe wa Kamati ya Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO), waandishi na wahariri habari, zimezaa matunda kwa kufanikisha kufanyika kwa mikutano mbalimbali na baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Waziri wa Habari Zanzibar, maafisa wa serikali, pamoja na wakuu wa wilaya na mikoa ya Zanzibar.
Mikutano hiyo imelenga kujenga uelewa, kuhamasisha maboresho ya sheria za habari na kuimarisha mazingira ya kazi kwa wanahabari, ulinzi na usalama pamoja na kuimarisha uhuru wa kujieleza visiwani Zanzibar.
“Tunajivunia mafanikio na hatua kubwa tuliyopiga kupitia juhudi za uchechemuzi na ushawishi unaofanywa na waandishi wa habari pamoja na wadau wa sekta ya habari. Juhudi hizi zimeongeza uelewa wa wanahabari katika kutetea haki zao pamoja na haki za wananchi kwa ujumla,” alieleza Zaina.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa TAMWA ZNZ, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchechemuzi TAMWA ZNZ, Bi. Shifaa Said Hassan, amewapongeza waandishi wa habari kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kuendeleza uchechemuzi wa sheria mbalimbali zinazominya uhuru wa habari Zanzibar.
“Ingawa programu hii inafikia tamati, waandishi wanaendelea na majukumu yao ya kila siku. Hivyo ni muhimu kuendeleza juhudi za uchechemuzi ili kuhakikisha sheria mpya na bora ya habari inapatikana ifikapo mwaka 2026,” alisisitiza Bi. Shifaa.
Washiriki wa mkutano huo pia walitoa maoni na mapendekezo ya kuboresha ripoti ya utekelezaji wa programu hiyo, huku wengi wakisisitiza umuhimu wa kuwa na sheria mpya ya habari itakayolinda uhuru wa vyombo vya habari, haki za waandishi, na uwajibikaji wa kitaaluma.
Aidha, baadhi ya waandishi walioshiriki walieleza kuwa programu hiyo imewasaidia kuchukua uamuzi wa kurejea vyuoni kwa ajili ya kujiendeleza kielimu, ili kuhakikisha kuwa wanakidhi vigezo vya kitaaluma na kuepuka kuzuiwa na masharti ya elimu iwapo sheria mpya itapitishwa.
Programu ya kupitia sheria za Habari Zanzibar (ARFEL) imetekelezwa na TAMWA-ZNZ kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo kuanzia Ogasti 2023 hadi Julai 2025, yenye lengo la kusaidia na kuimarisha mapitio ya sheria za habari nan a kuimarisha huru wa kujieleza.
Next
« Prev Post
« Prev Post
Previous
Next Post »
Next Post »
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
EmoticonEmoticon