SERIKALI YALIPA FIDIA YA SHILINGI MILIONI 999 KWA WANANCHI 103 WA DODOMA KWA MIRADI YA MAJI

August 13, 2025



Afisa Mazingira kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Ambrosi Siril akimsaidia mzee Peter Mazengo kusaini katika daftari la fidia katika eneo la Zuzu Nala jijini Dodoma ambao maeneo yao yamechukuliwa na DUWASA. Agosti 11,2025
DODOMA, Agosti 12, 2025

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wizara ya Maji, imekamilisha zoezi la ulipaji wa fidia yenye jumla ya Shilingi Milioni 999 kwa wananchi 103 ambao ardhi yao ilitwaliwa katika maeneo ya Nzuguni, Zuzu Nala, Nala Chihoni na Kibaigwa kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya maji inayotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA).

Ulipaji wa fidia hizo, umeongozwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na DUWASA, Wizara ya Ardhi na Viongozi wa Serikali za Mitaa wa maeneo husika, ambapo kwa eneo la Nzuguni, Wananchi 24 wamelipwa fidia ya Shilingi Milioni 148 tarehe 07 Agosti, 2025,.


Aliyekuwa Mbunge wa Chato, Dkt. Medard Kalemani (kushoto), akipokea hundi kutoka kwa Muhasibu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Getrude Mosha wakati wa zoezi la ulipaji fidia kwa wakazi wa Zuzu Nala jijini Dodoma ambao maeneo yao yamechukuliwa na
DUWASA. Agosti 11,2025


Alitaja wengine kuwa ni Zuzu Nala Wananchi 51 ambao wamelipwa fidia ya Shilingi Milioni 594 Agosti 11, 2025, Nala Chihoni Wananchi 7 ambao walilipwa fidia yao ya Shilingi Milioni 58 tangu mwezi Aprili, 2025 na Kanda ya Kibaigwa Wananchi 23 wamelipwa fidia ya Shilingi Milioni 197 na kukamilisha zoezi hilo Agosti 12, 2025.


Muhasibu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Getrude Mosha (kulia) akizungumza na mkazi wa Nzuguni wakati wa zoezi la ulipaji fidia kwa wakazi wa Nzuguni jijini Dodoma ambao maeneo yao yamechukuliwa na DUWASA. Agosti 11,2025


Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa kiasi hicho cha fedha kwa wananchi waliyotoa ardhi yao kupisha utekelezaji wa miradi ya maji.

 Mkazi wa Nzuguni, Benjamini Elias akisaini katika daftari la fidia wakati wa zoezi la ulipaji fidia kwa wakazi wa Nzuguni jijini Dodoma ambao maeneo yao yamechukuliwa na DUWASA. Agosti 11,2025


"DUWASA, kwa niaba ya Wananchi wa maeneo ya Nzuguni, Zuzu Nala, Nala Chihoni na Kibaigwa, inaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita na Wizara ya Maji kwa juhudi zao kubwa na ufanisi katika kuhakikisha ulipaji wa fidia kwa wakati kwa wananchi wetu," alisema Mhandisi Aron.

"Hatua hii ni muhimu sana kwa maeneo yaliyotekelezwa na yanayoendelea na utekelezaji wa miradi ya maji ya kimkakati katika Jiji la Dodoma na Kanda ya Kibaigwa, hii inaonesha dhamira ya Serikali katika kulinda haki za wananchi wakati wa kutekeleza miradi ya maendeleo." Amesma Mhandisi Aron.


Afisa Mazingira kutoka Wizara ya Maji, Moses Mgalla, akizungumza na wananchi wa Kibaigwa ambao maeneo yao yamechukuliwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) wakati wa zoezi la ulipaji fidia kwa wakazi wa Mji wa Kibaigwa jijini Dodoma. Agosti 12,2025


Kwa upande wa wakazi wa Kibaigwa, Bi. Josephina Paulo ameishukuru serikali kwa kuwasikiliza na kuwalipa fidia. Ameiomba serikali kwa kuwaona wanyonge na kuwafikia wengine ambao bado hawajalipwa wanasubiri kulipwa.

Naye Bwa. Yohana Mwarabu ameshukuru serikali kwa kumjali na kumlipa kwani sasa ataenda kujenga nyumba nyingine ili aweze kuishi na familia yake kwani awali hakuwa na matumaini lakini kwa sasa anaamani.

Fidia hiyo ni sehemu ya maandalizi ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maji inayotekelezwa na Serikali kupitia DUWASA iliyokusudiwa kuboresha upatikanaji wa majisafi na huduma za usafi wa mazingira ka wakazi wa jiji la Dodoma na maeneo mengine yanayohudumiwa na DUWASA.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »