Showing posts with label elimu. Show all posts
Showing posts with label elimu. Show all posts

CRDB Bank Foundation, StartHub Africa zaungana kuwawezesha wanafunzi wa vyuo vikuu

June 13, 2025 Add Comment

 

Meneja Uendelezaji Biashara Changa wa CRDB Bank Foundation, Sharron Nsule akitoa elimu ya ujasiriamali kwa wanafunzi walioshiriki semina katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Dar es Salaam, Tanzania – June 2025: Katika kuendeleza jitihada za kuinua ujasiriamali na kuwawezesha wanafunzi wabunifu, Taasisi ya CRDB Bank Foundation kwa kushirikiana na StartHub Africa imevitembelea vyuo vikuu vitatu nchini na kutoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa wanafunzi wanaopenda kumiliki biashara baada ya masomo yao.

Ushirikiano huo unaotekelezwa kupitia programu ya “Uni Launch and Scale” tayari umewafikia zaidi ya wanafunzi 1,000 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Iringa na Taasisi ya Uhasibu Arusha (AIA) na kuwapa fursa ya kupata walezi wa kibiashara na mitaji wezeshi kutoka CRDB Bank Foundation.

Akizungumzia mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa amesema vyuo hivi vitatu ni mwanzo tu kwani lengo lililopo ni kuwafikia wanafunzi wengi zaidi na kuwawezesha ili wanapohitimu au wakai wanaendelea na masomo yao waanze kushiriki shughuli za kuujenga uchumi baada ya kuwapa elimu ya fedha, mafunzo ya ujasiriamali na uhakika wa kupata mtaji wezeshi.

“Lengo letu ni kuamsha ari ya ujasiriamali iliyomo ndani ya wanafunzi wetu wa vyuo vikuu na kutoa mazingia rafiki kwao kuanzisha biashara zitakazoajiri vijana wenzao badala ya wao wenyewe kuwa waombaji wa kazi wakihitimu. Kupitia ushirikiano huu tunajenga kizazi cha vijana waliowezeshwa kushiriki kuujenga uchumi wa taifa letu,” anasema Tully.

Katika vyuo vitatu ambako wataalamu wa CRDB Bank Foundation na StartHub Africa wamepita, jumla ya biashara 30 zinazomilikiwa na kuendeshwa na wanafunzi zitachaguliwa baada ya kukaguliwa ili kuingizwa kwenye mpango maalumu wa mafunzo ya usimamizi na uendeshaji biashara, utayari wa kifedha na utimamu wa bidhaa.

“Kwa kushirikiana na StartHub Africa pamoja na vyuo vikuu hivi, tunaamini tunaendeleza juhudi za kukuza ubunifu hasa wa kidijitali miongoni mwa wanafunzi wetu hivyo kujenga msingi imara wa biashara zinazoweza kukua na kuwanufaisha wananchi wengi,” amesema Tully.

Programu ya Uni Launch and Scale ambayo CRDB Bank Foundation inashirikiana na StartHub Africa kuitekeleza inalenga kuwawezesha wanafunzi wa vyuo vikuu kutekeleza uwekezaji wanaoukusudia kwa kuwapa mafunzo, ulezi wa kibiashara na uwezeshaji wa mitaji kupitia Programu ya Imbeju iliyojielekeza kuwainua vijana, wanawake na makundi maalumu.

Meneja Programu wa StartHub Africa, Zagaro Emanuel anasema katika ushirikiano huu wanakusudia kuwawezesha vijana wengi wabunifu kupitia mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha hivyo kuchangia kuujenga uchumi na kusukuma mbele maendeleo ya Tanzania.

“Tunawahamasisha wanafunzi na wahitimu wa vyuo vikuu, tunawandaa waanzilishi wapya wa biashara watakaosaidia kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kuimarisha ujasiriamali nchini kwa kushirikiana na vyuo vikuu, wawekezaji na wawezeshaji. Tukiwa pamoja na Taasisi ya CRDB Bank Foundation, tunaamini tutafika mbali na kuwajumuisha wanafunzi wengi zaidi nchini,” anasema Emanuel.

Meneja huyo anaongeza kwamba programu hiyo inawapa wanafunzi jukwaa la kujitangaza katika soko la ndani, kitaifa na kimataifa na wanapowasilisha mawazo ya miradi yao, wanajiweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kuvutia mitaji huku vyombo vya habari vikiwarahisishia kujulikana kwa biashara zao hivyo kujiongezea umanifu kwa wadau ambalo ni jambo jema kwa kila biashara.

DKT.BITEKO AFURAHISHWA NA UTATUZI CHANGAMOTO ZA ARDHI MONDULI

April 24, 2025 Add Comment


📌 Azindua Shule ya Sekondari Migungani, awataka wanafunzi kutunza miundombinu


📌 Asema Serikali yajipanga kujenga mradi mkubwa wa umeme Monduli


Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameupongeza uongozi wa Wilaya ya Monduli kwa jitihada zao za kutatua migogoro ya ardhi wilayani humo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la  Serikali la  kuwataka viongozi kutatua changamoto za wananchi katika maeneo yao.

Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo Aprili 23, 2025 wilayani Monduli, mkoani Arusha wakati akihutubia wananchi mara baada ya kuzindua Shule Mpya ya Sekondari ya Migungani iliyopo wilayani humo.


“Naomba kuwapongeza tena uongozi wa Wilaya ya Monduli kwa kuendelea kufanya kazi nzuri sana hapa wilayani kwa maslahi mapana ya wananchi wa Monduli. Nimejulishwa kuwa, mmefanya mengi mno ikiwemo utatuzi wa changamoto na migogoro ya ardhi hapa wilayani. Nimejulishwa kuwa sehemu kubwa ya changamoto hizi mmefanikiwa kuzitatua hongereni sana,” amesema Dkt. Biteko.

Ameipongeza pia kamati ya kutatua kero za wananchi inayoongozwa na Mkuu wa Wilaya ikiwa na wataalamu mbalimbali ambayo imejiwekea utaratibu wa kupokea kero kutoka kwa wananchi na kuzipatia ufumbuzi, ambapo ameitaka pia iratibu zoezi la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya ardhi.

Akiwa shuleni hapo, Dkt. Biteko amewapongeza wananchi kwa kujenga shule hiyo ya Sekondari Migungani na kufikia asilimia 85 ya ujenzi huku Serikali ikichangia shilingi milioni 500.


“ Sote tunafahamu kuwa, elimu ni msingi mkubwa wa maendeleo. Sisi wana Monduli tayari tunayo shule yetu hii ambayo imeshakamilika. Hii ni miongoni mwa shule zilizopo Wilayani hapa ambazo zitaendelea kutupatia elimu kwa vijana wetu,” amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa Shule hiyo itakuwa na uwezo wa kuwa na wananfunzi 400 na hivyo amewataka wanafunzi kutunza miundombinu sambamba na kujifunza kwa bidi ili wajiandae kuwa wazalendo na raia wema huku wakiwa na uwezo wa kutafuta majibu ya matatizo watakayokumbana nayo.


Kuhusu miradi ya umeme wilayani humo, amesema kuwa mwaka huu Serikali inatarajia kujenga mradi mkubwa wa umeme kwa lengo la kuuongezea nguvu umeme  unaopatikana ili uweze kufika  Loliondo na kusaidia wilaya hiyo kuwa na  umeme wa uhakika.

Aidha, Dkt. Biteko amezungumzia maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano kwa kuwataka Watanzania kuenzi muungano huo kwa kujenga Taifa moja kwa kushikamana  na kufanyakazi kwa pamoja kwa kushirikiana.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Mhe. Festo Kiswaga amesema kuwa Wilaya hiyo ni tegemeo kwa Chama Cha Mapinduzi na wamekuwa wakishirikiana na wananchi katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo.

Pia, amesema Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo barabara, hospitali, shule na kuwa Wilaya hiyo ni kati ya wilaya zinazofanya vizuri katika elimu na huku akimshukuru Rais Samia kwa kuwekeza katika elimu nchini.


MWISHO

WAISHUKURU TAASISI YA UMOJA WA WASAIDIZI WA SHERIA UWASHEM KUWAWEZESHA KUTATUA MIGOGORO BAINA YA WAVUVI NA WAKULIMA WA MWANI

April 07, 2025 Add Comment

 


WANANCHI wanaofanya shughuli za  Uvuvi na Wakulima wa Zao la Mwani wanaoishi katika kijiji cha Mwaboza wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga wameishukuru taasisi ya Umoja wa wasaidizi wa Sheria 'UWASHEM' kwa kuwawezesha kutatua mgogoro baina yao kutokana na matumizi ya rasilimali bahari ambapo kupitia elimu waliyoipata imewawezesha kuwaunganisha.


Awali wakizungumza katika mdahalo wa pamoja  ulioandaliwa na taasisi hiyo kwa lengo la kutambua changamoto zilizopo baina yao Kila mmoja ameonekana kumshutumu mwingine kuwa chanzo cha mgogoro kwa kile walichoeleza kuwa wamekuwa wakigombania maeneo hali iliyopelekea kukosa maelewano na hatimaye kuwaingiza kwenye mgogoro.

Wakizungumza baadhi yao wamesema kuwa pamoja na elimu waliyoipata kupitia shirika la UWASHEM' ni vyema Serikali ikatenga maeneo maalum ili kuwasaidia wananchi hao kufanya shughuli zao bila bughuza  na hatimaye kuendelea kujipatia kipato Chao cha Kila siku

Mratibu wa miradi kutoka shirika la UWASHEM' Swalehe Sokolo amesema kuwa  kupitia mradi huo wanaoutekeleza imesaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto baina ya Wavuvi na Wakulima wa Zao la Mwani ambapo pia wameweza kuwaunganisha na viongozi wa Serikali.

Kwa upande wake mratibu wa mradi wa KUJENGA AMANI PAMOJA kutoka shirika la shirika la We World  Zacharia Msabila amesema wanafanya kazi na  taasisi zilizopo karibu na jamii ambapo kupitia ufadhili wanaoutoa itasaidia kufikia malengo waliyoyatarajia.

Diwani wa kata ya Moa Staruki Njama amekiri uwepo wa migogoro ya muda mrefu biana ya Wakulima wa Zao la Mwani na Wavuvi katika kijiji cha Mwaboza ambapo shirika la UWASHEM' limekuja kuleta suluhisho kupitia elimu waliyoitoa ambapo amewapongeza kwa jitihada walizozifanya huku akisisitiza  wananchi kuendelea kufuatia na kutekeleza Sheria zilizowekwa.

Shirika la umoja wa usaidizi wa Sheria Mkinga "UWASHEM'' linatekeleza mradi wa KUJENGA AMANI  PAMOJA katika wilaya hiyo kwa kushirikiana na shirika la 4H Tanzania  ukifadhiliwa na shirika la We World kwa lengo la kuleta amani baina ya wananchi kutatua changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kupelekea uvunjifu wa amani.

VETA TANGA WAADHIMISHA MIAKA 30 YA KUANZISHA KWAKE KWA KUFANYA UKARABATI SHULE YA MSINGI CHANGA

March 16, 2025 Add Comment


Na Oscar Assenga,TANGA

CHUO cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Jijini Tanga katika kuadhimisha miaka 30 ya kuanzishwa kwake wamefanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kufanya ukarabati wa majengo ,Miundombinu ya Umeme ,Tehama pamoja na kwashonea sare wanafunzi wa Shule ya Msingi Changa ya Jijini Tanga.

Akizungumza kuhusu maadhimisho hayo Mkuu wa VETA kituo cha Tanga,Gideon Lairumbe alisema kwamba wameamua kuadhimisha katika shule hiyo kutokana na kwamba ni miongoni mwa wanufaika wa maadhimisho ya VETA ambayo kitaifa kilele chake kitafanyika Jijini Dar es salaam kuanzia Machi 17 hadi 21 mwaka huu mgeni rasmi anatarajiwa kuwa waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Alisema kwa ngazi ya kituo cha Tanga,VETA imefanya ukarabati darasa la awali kujenga sakafu ya nje ya shule,mfumo wa umeme,Tehama na kuziba maeneo hatarishi maeneo hatarishi ya mmomonyoko wa udongo wakati wa mvua .

Eneo jingine ambalo shule hiyo imenufaika na VETAni kuwashonea sare wanaf unzi 150,kupiga rangi na kukarabati mfumo wa jiko la kupikia zikiwamo sufuria.

Shule nyingine iliyonufaika na VETA katika maadhimisho hayo ni ya Msingi Juhudi wa mamambayo wanafunzi wenye mahitaji maalumu wameshonewa sare na kwa upande wa Mama lishe katika mitaa mbalimbali wamepewa kofia na vizibao vya kuwahudumia wateja.

“Tumefanya hivi ikiwa ni jithada za VETA kurejesha imani kwa jamii ambayo imekuwa ikiihudumia kwa kipindi cha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake lakini pia kuwavuta vijana kujiunga katika mafunzo yake ambayo yamesaidia kwa kiasi kikubwa kutoa ajira”amesema Lairumbe.

Yussuph Ilias ambaye ni mzazi wa wanafunzi wawili wanaosoma shule ya Msingi Changa amesema ukarabati uliofanywa na VETA umesaidia kwani imebadilika na kuwa ya kisasa na kuwawezesha awanafunzi kusoma bila wasiwasi.

“Kwa mfano upande wa baharini shule ya Changa inapakana na bahari ya Hindi..kule chini kulikuw na mmompnyoko ambao ulikuwa ukitutia wasiwasi wazazi kuhusu usalama wa watoto,lakini VETA wameweka vifusi na hali imekuwa nzuri”amesema Ilias.

Makamu Mwenyekiti wa wanafunzi wa Chuo cha VETA Tanga,Mariam Hashim amewaomba wazazi kuwapeleka vijana wao waliohitimu shule za Sekondari na vyuo mbalimbali ili kupata mafunzo ya ufundi yatakayowasaidia kujiajiri.

“Mfano ni mimi nimehitimu chuo kikuu lakini nimeamua kuja VETA kupata ujuzi wa ufundi wa umakenika na kabla sijamaliza mwaka wangu wa pili tayari kuna mashirika matatu yamenifuata na yameahidi kunipa kazi”amesema Mariam.

KAMPUNI YA DNATA NA EMIRATES LEISURE ZATOA MSAADA WA VIFAA VYA SHULE ZANZIBAR

January 26, 2025 Add Comment



Wafanyakazi wa Kampuni za DNATA na Emirates Leisure za Zanzibar wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari za Kijiji cha Kendwa baada ya kupatiwa vifaa vya shule Januari 23, 2025.

................................................ 

Na Dotto Mwaibale 

KAMPUNI ya DNATA na Emirates Leisure za Zanzibar zimetoa vifaa vya shule kwa Shule za Msingi na Sekondari za Kilindi  kwa ajili ya kusaidia jamii zenye uhitaji. 

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada huo Kijiji cha Kendwa kilichopo Wilaya ya Kaskazini A Mkoa wa Kaskazini, Mwakilishi wa kampuni ya Emirates Leisure  Msokolo Layya alisema wameamua kutoa sehemu ya fedha zao kwenye eneo la elimu ambayo ndio msingi wa maisha na kuwa msaada huo umewafikia wanafunzi 240. 

“Kampuni hizi zimeanzisha mpango wenye lengo la kutoa nyenzo muhimu za kujifunzia watoto ili kuwajengea uzoefu na kuwainua kitaaluma,” alisema Layya. 

Layya alitaja vifaa hivyo kuwa ni kalamu za kuandikia, vifutio, madaftari, mikebe yenye vifaa vya kucholea na vingine vinavyofanana na hivyo. 

Layya alisema kampuni hizo zitaendelea kusaidia wahitaji na kuwa mpango huo ni endelevu na tayari wamekwisha ratibu ratiba ya kufanya hivyo kwa mwaka mzima. 

Alisema kampuni hizo zinafanya hivyo ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kusaidia makundi yenye uhitaji na shughuli mbalimbali za kijamii. 

Akizungumza katika hafla hiyo Meneja wa Kampuni ya  Emirates Leisure, Paul Attallah alisisitiza kuendelea kudumisha ushirikiano baina ya kampuni hizo na Serikali ili kutoa huduma kwa wananchi wa Zanzibar hasa katika sekta ya elimu.

Wanafunzi hao wakiwa na vifaa vya shule walivyo kabidhiwa.
Vifaa hivyo vikikabidhiwa kwa wanafunzi hao. Kushoto ni Mwakilishi wa kampuni ya Emirates Leisure  Msokolo Layya.
 

RAIS MWINYI:MIAKA 61 YA MAPINDUZI NCHI INA MAENDELEO MAKUBWA

December 21, 2024 Add Comment

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amebainisha kuwa katika miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar nchi imeshuhudia hatua kubwa ya maendeleo katika miundombinu mbalimbali ikiwemo elimu, afya, umeme, maji, barabara, teknolojia, madaraja  na bandari  katika miradi yote hii wahitimu wa Taasisi hii ni miongoni mwa wahandisi ambao waliotoa mchango mkubwa sana kufanikisha maendeleo hayo.

Rais Dk.Mwinyi ameyasema hayo kwenye mahafali ya 10 ya Taasisi ya  Sayansi na Teknolojia ya Karume, Mbweni, Mkoa wa Mjini Magharibi tarehe 21 Disemba 2024.


Aidha, Rais Dk.Mwinyi amewasisitiza wahitimu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume, kuitafsiri elimu waliyoipata kwa vitendo badala ya nadharia ili kutoa mchango wao kwa maendeleo ya nchi.


Rais Dk.Mwinyi amesema Serikali itaendelea kutambua umuhimu wa taasisi hiyo kama chachu ya maendeleo kwa kuzalisha wataalamu wenye ujuzi katika sekta mbalimbali.

Halikadhalika Rais Dk.Mwinyi amesema kuanzishwa kwa Taasisi hiyo ni jitihada ya kutafsiri kwa vitendo dhamira ya elimu ya amali na ufundi na kuwapa mbinu wananchi za kujitegemea ikiwa ni hatua muhimu ya ilani ya Chama cha Afro Shirazi iliyokuwa na dira na malengo ya muda mrefu ya kuandaa rasilimali watu kwa kuitumikia nchi na kusukuma mbele maendeleo. 

Hatua  hiyo inakwenda sawasawa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020 - 2025 inayoweka mkazo kwa vijana kupewa elimu ya amali na ufundi ili wajitegemee badala ya kusubiri ajira chache zilizoko katika mfumo wa Serikali.

Rais Dk.Mwinyi ameeleza  kuwa tangu kuanza kwa Awamu ya Nane, Serikali imeipatia taasisi hiyo, miradi mikubwa miwili ikiwemo kuwajengea uwezo Vijana Kujiajiri na Kuajirika katika Sekta ya Uchumi wa Buluu pamoja na mafunzo katika sekta ya ufundi na sayansi na teknolojia yenye viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa ambayo kumalizika kwake kutaimarisha miundombinu ya Taasisi hiyo pamoja na rasilimali watu.




TUWAINUE WABUNIFU WAZAWA KUWANADI KIMATAIFA-DKT BITEKO

December 16, 2024 Add Comment



*📌 Asisitiza Mifumo iboreshwe kuakisi Maendeleo*


*📌 Serikali kuweka Mazingira wezeshi kwa wadau wa STARTUPs*


*Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati*


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa pamoja na jitihada za kuwainua wabunifu wawekezaji nchini, bado kuna umuhimu mkubwa wa kuwawezesha wabunifu wetu kukua zaidi ndani na nje ya mipaka ya nchi.


Dkt. Biteko amesema hayo leo Desemba 16, 2024 Jijini Dar es Salaam alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua Kongamano la Uwekezaji wa Kampuni Bunifu (STARTUPs)



Amesema kuwa Tanzania imerekebisha mifumo mingi ili kuwezesha ubunifu na uwekezaji wa moja kwa moja nchini kuleta maendeleo, suala ambalo tumeona likifanikiwa na kwahiyo linahitaji kupaliliwa na kuungwa mkono kwa matokeo chanya.


“Nimewasikiliza wanakongamano na kupitia majadiliano haya ni wazi kwamba bado kuna namna ya kuboresha zaidi mifumo yetu ya usimamizi na utawala ili kuhakikisha Wabunifu wanapata nafasi nzuri zaidi.” amesema na kuongeza kuwa, Tunatamani kuona Watanzania wanashiriki katika kukuza uchumi wa nchi yao na pengine kuazimwa katika nchi nyingine.” amesema Dkt. Biteko



Amesema wapo baadhi ya Watanzania wanaofanya shughuli zao nje ya Nchi ambao wanaiwakilisha vema Tanzania kutokana na kufanya kazi kwa kuzingatia misingi iliyowekwa katika nchi hizo na hivyo kuwataka wabunifu wawekezaji kuiga mfano huo.


Aidha, Dkt. Biteko amesema kuwa Maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yako wazi na kwa nyakati mbalimbali amekuwa akijipambanua kuhusu uwezeshaji wa makundi mbalimbali wakiwemo wabunifu wawekezaji.

 


“kwa kutekeleza maono ya Rais, ni muhimu kuwasikiliza, kuwaamini na kufanyia kazi maoni na bunifu zao ili kuboresha mazingira yatakayo wawezesha kutekeleza Bunifu zao na kupata fursa ndani na nje ya Nchi”.


Naye, Naibu Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo akimwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, Prof. Kitila Mkumbo amesema Serikali imekuwa ikizingatia suala la uwezeshaji kwa Wabunifu Wawekezaji ikiwa ni pamoja na kupokea maoni yao kupitia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.


Nyongo ameongeza kuwa, Serikali imeboresha mazingira ya biashara kwa kupunguza gharama za biashara ili kuwawezesha wabunifu kutimiza ndoto zao.



Kwa upande wake, Waziri Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry Silaa amesema Wizara imeandaa mazingira ya kuwawezesha Wabunifu kufanya majaribio ya kazi zao kupitia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).


Amesema Serikali imejenga vituo vya ubunifu vinane (8) katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kuwawezesha Wabunifu kujiandaa na hatimaye kupata ajira katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii.


Awali,


Mkurugenzi Mtendaji wa TSA, Zahoro Muhaj amemshukuru Rais Samia kwa maono yake ya kuwatambua na kuwawezesha wabunifu ili waweze kuchagiza maendeleo ya nchi.


“ Tunaomba salam zetu zifikishwe kwa Mheshimiwa Rais, ambaye amekuwa akitubeba na kusafiri nasi katika nchi mbalimbali ili tupate uzoefu na kukua kama mtu kama mtu mmoja mmoja na baadae kama Taifa,” amesema Muhaj. 


Kwa upande wake, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Nelson Bonephace ameishukuru Serikali kwa jitihada za kuwawezesha wabunifu wawekezaji kukua.


Amesema katika kipindi cha mwaka 2020 hadi sasa zaidi ya dola za kimarekani Milioni 49 zimetolewa ambazo zinatumika kujenga Kampasi mpya za Kagera, Zanzibar na Lindi.


Mwisho.

MKUU WA CHUO CHA IFM APONGEZWA KWA KUBUNI MIKAKATI MBALIMBALI

December 16, 2024 Add Comment

 Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Benk ambaye pia ni mwanajumuiya wa Chuo Cha Usimamizi wa Fedha (IFM) (Alumni) Abdulmajid Nsekela amempongeza Mkuu wa chuo hicho Profesa Josephat Lotto na timu yake kutokana na kubuni mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuboresha elimu nchini.


Nsekela ameyazungumza hayo wakati wa hafla ya chakula cha jioni ya wanafunzi waliosoma zamani katika chuo hicho ,iliofanyika usiku wa kuamkia leo jijini Dodoma.

Nsekela amesema mkakati wa kushawishi wanafunzi wapende somo la hisabati lakini pia kukifahamu chuo hicho ni mzuri kutokana na kwamba utaongeza wigo wa wanafunzi kujiunga na chuoni hapo kusoma kozi mbalimbali zinazotolewa.

Aidha alisema wao kama Alumni watashirikiana pamoja na IFM ili kuhakikisha chuo hiko kinazidi kutanua wigo wa utoaji elimu ndani na nje ya nchi ili kuzalisha wataalamu wengi wa masuala ya fedha.

"Nampongeza mkuu wa chuo kutokana na kubuni mikakati mbalimbali ya kuboresha chuo hiko,"alisema Nsekela.

Kuhusu fedha milioni 52.8 zinazohitajika kwa ajili ya mkakati wa kupeleka conter book shuleni ili kushawishi wanafunzi kupenda kusoma hisabati na kuifahamu IFM,Nsekela aliendesha harambee kwa Alumni hao,ambapo ahadi zilipatikana shilingi milioni 36,huku fedha tasilimu zilipatikana shilingi milioni nane.

Kwa upande wa Mkuu wa chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM),Profesa Josephat Lotto amewaomba Alumni waliosoma katika chuo hiko,ambao wapo katika ofisi mbalimbali,kuhakikisha wanawasimamia wanafunzi wanaoenda kufanya mafunzo kwa vitendo ili kupata uzoefu,badala ya kuwatuma kukoroga chai na kubeba mafaili.

Profesa Lotto amesema wanafunzi hao wanapoenda katika ofisi mbalimbali kwa ajili ya kufanya mafunzo kwa vitendo ya fani walizosomea wengi wanaishia kutumwa mafaili na kukoroga chai jambo linalopelekea kushindwa kupata kile alichokusudia na kurudi chuoni akiwa hana kitu.

"Hili suala linasikitisha sana kwa sababu wanafunzi wanarudi chuoni wakiwa hawajapata kitu,naomba nyie kama alumni mliopo katika ofisi mbalimbali kuwasaidia wanafunzi hao ili wakihitimu waweze kuajirika au kujiajiri wao wenyewe,"alisema Profesa Lotto.

Alisema wao kama wadau,wakiamua kuwasimamia wanafunzi hao,basi itachangia kwa kiasi kikubwa wanafunzi hao,kupata uzoefu wa kutosha na kufanya vizuri hapo baadae katika sehemu ya vitendo watakapoajiriwa au kujiajiri wao wenyewe.

Kutokana na hilo,ametoa rai kwa alumni wa IFM kuwa sehemu ya mkakati wa chuo hiko wa kuanzisha platform ambayo itahusisha waajiliwa waliomaliza IFM kutoka taasisi tofauti,pamoja na wanafunzi ili kuwasaidia kufanya majaribio kupitia platform na kupata kile walichokusudia.

"Wanafunzi waliofikia muda wakwenda kufanya mafunzo kwa vitendo,wataingia kwenye platform hiyo pamoja na waajiri,hii itakuwa imesaidia kufanya majaribio kwa vitendo kupitia platform,"alisema Profesa Lotto.

Mbali na hilo alisema katika kuisapoti serikali kuzidi kuinua kiwango cha elimu hapa nchini,Chuo cha IFM kimebuni mkakati wa kupeleka madaftari yaliyo na nembo ya chuo hiko,katika shule mbalimbali hapa nchini,ili wanapohitimu wajue kuna chuo hiko.

Profesa Lotto alisema lengo la kufanya hivyo ni pamoja na kuwashawishi wanafunzi kupenda somo la hisabati ambalo katika kozi nyingi zinazotolewa hapo ni lazima somo hilo lisomwe.

Alisema kwa kuanzia wameanza na shule 184 kutoka wilaya 40 za mikoa sita,ambapo alisema wanahitaji sh milion 52.8 ili kufanikisha mkakati huo wa kushawishi wanafunzi wapende somo la hisabati

DIWANI PEREMBO AISHUKURU SERIKALI KUWAPA ZAIDI YA MILIONI 300 KWA AJILI YA UJENZI WA SHULE YA SEKONDARI MPYA

December 14, 2024 Add Comment




Na Oscar Assenga, TANGA.

DIWANI wa Kata ya Majengo Jijini Tanga (CCM) Salim Perembo ameishukuru Serikali kutoka zaidi ya Milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Chuma itakayokuwa mkombozi kwa wanafunzi wanaosoma mbali na kata hiyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa mradi huo ambapo shule hiyo itajengwa Ghorofa ilisema kwamba ujenzi huo ni miongoni mwa mipango yake kuhakikisha wananchi wa kata hiyo wanapata shule ya Sekondari.

Alisema kwamba ujenzi huo ni moja ya mambo makubwa walioyafanya katika Kata hiyo ili kuhakikisha wanafunzi wanatimiza ndoto zao za kupata elimu bora bila uwepo wa changamoto yoyote ile.

Aidha aliongeza kwamba hayo ni moja ya makubaliano na wananchi baada ya kupata ridhaa ya kuwaongoza ni kuwajengea soko la mlango wa chuma,shule ya Sekondari Chuma,watajenga barabara za lami,watatia taa kwenye maeneo yao ili kuondoa giza,mikopo na kukarabati shule za msingi nne ili ziweze kuwa na muonekana mzuri.

Alisema wakati anapata ridhaa ya kuwaongoza wananchi shule ya Masiwani na Chuma mvua zilipokuwa zinanyesha maji yanaingia madarasani lakini wamekuja na kuhakikisha wanamaliza changamoto hizo na wanashukuru kilio cha wananchi kimepata ufumbuzi asilimia 70 mpaka 80.

Diwani huyo alisema tayari shule ya Msingi Masiwani imerudi katika hali yake kawaida na imekuwa shule mpya na wamejenga shule mpya ya msingi Chuma ambao mdhibiti na mkaguzi wa elimu amefika na kuidhinisha kwamba shule hiyo ibadilishwe iwe sekondari.

Alisema kwamba haiwezekani kufuta jina la shule ya Msingi Chuma kwa sababu hivyo kihistoria hivyo wakaona wajenga shule mpya kwa hiyo walipata na fedha karibia milioni 300 ambazo ziliingizwa kwa ajili ya soko la Mlango wa Chuma lakini baada ya kupata wafadhili Green Smart City fedha hizo zikawepo kwa ajili ya mambo mengine wakazigeuza kwa ajili ya ujenzi mpya wa shule ya Msingi Chuma.

Diwani huyo alisema fedha hizo ndio zilikarabati eneo mbadala baada ya wafanyabiashara soko la Mlango wa chuma kuhamishiwa eneo la CCM hivyo walimega fedha kukarabati eneo na kujenga chuo kipya na wakaweka umeme na maji na wakakarabati jengo kwa ajili ya mamantilie.

Alisema fedha ambazo zilibakia wamejenga shule mpya ya Chuma mpya yenye madarasa tisa na ofisi na vyoo vyenye matundu 20 hivyo watambue kwamba wamejenga shule mbili mpya ya kwanza ni shule ya Msingi Chuma na shule mpya ya Sekondari ujenzi wake utakaoanza.

Awali akizungumza Afisa Tarafa wa Tarafa ya Ngamiani Kati Leonadi Sembe aliwataka wananchi wa eneo la Majengo Jijini Tanga kunakojengwa shule Mpya wa Sekondari Chuma kuwa sehemu ya kukamilika kwa mradi huo na wasiwe miongoni mwa watu watakaofanya hujuma za aina yoyote ile.

Alisema wakati wa ujenzi wa mradi huo kutakuwa na shughuli mbalimbli ikiwemo vifaa ambavyo vitakuwa vikitumika hivyo wananchi wanapaswa kuwa sehemu ya kukamilisha mradi huo

“Ujenziwa ya Sekondari ya Ghorofa ilikwa stori sasa sio stori tena ninachowaomba wananchi tuwe sehemu ya kukamilisha mradi` huo na tusiwe miongoni mwa watu watakaofanya hujuma za aina yoyote ile kwani kuna tabia kunapokuwa na miradi kama hii vijana ambao sio waaminifu wamekuwa wakitumia hiyi fursa kuiba baadhi ya vifaa”Alisema

Aidha aliwaambia kwamba Serikali, Viongozi wa Tarafa ,Kata na wilaya kwa ujumla macho yao yapo kwenye mradi huo hivyo hawatamvumilia mtu wa aina yotote ambaye atabainika au na viashiria ama kutaka kufanya tukio la kutaka kuhujumu mradi huo.

“Eneo hili limekuwa kitovu cha elimu sidhani kama kuna kata ina shule katika eneo moja kuwa na shule hizo eneo hilo kama tumeamua kulifanya kuwa la elimu hakuna sababu ya vijana wanaovuta bangi na kutumia madawa ya kulevya kuendelea kuwepo kwenye maeneo hayo”Alisisitiza.

Alisema kwa sababu wameshadhamiria kulifanya eneo hilo kuwa la elimu huku akitoa wito kwa vijana wanaozurura maeneo hayo na kuhatarisha usalama wa watoto hivyo niwaeleze eneo hilo sio rafiki kwa mambo wanayo yafanya kwani wamedhamiria watoto wawe salama

Naye kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo Rehema Ally alisema wamelipokea kwa furaha ujenzi wa shule hiyo kwa maana kilikuwa ni kilio chao cha muda mrefu kutokana na kutokuwa na eneo la kujengea shule

Alisema lakini kwa sasa limepatikana na hivyo ujenzi huo utakapokamilika utawezesha wanafunzi kuacha kutembelea umbali mrefu kwende shule za jirani badala yake watasoma ndani ya kata hiyo ikiwemo kuepukana na vitendo vya vishawishi.

Mwisho.




SERIKALI KUENDELEA KUJENGA MIUNDOMBINU YA HUDUMA ZA AFYA

December 12, 2024 Add Comment

 


Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga akitoa vyeti kwa Wahitimu Katika mahafali ya sita ya Chuo Cha Afya na Sayansi Shirikishi Excellent yaliyofanyika Kibaha Mkoani Pwani leo Desemba 12, 2024.



Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga akizungumza  Katika mahafali ya sita ya Chuo Cha Afya na Sayansi Shirikishi Excellent yaliyofanyika Kibaha Mkoani Pwani leo Desemba 12, 2024.


Matukio Mbalimbali Katika mahafali ya sita ya Chuo Cha Afya na Sayansi Shirikishi Excellent yaliyofanyika Kibaha Mkoani Pwani leo Desemba 12, 2024.

Na Mwandishi Wetu,Pwani

KATIKA kuimarisha huduma za afya serikali inaendelea na juhudi za ujenzi wa zahanati na vituo vya afya ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu na huduma za afya katika hospitali zote kuanzia ngazi za chini hadi hospitali za rufaa.

Hayo yamesemwa na Naibu waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Omary Juma Kipanga Katika mahafali ya sita ya Chuo Cha Afya na Sayansi Shirikishi Excellent yaliyofanyika Kibaha Mkoani Pwani leo Desemba 12, 2024. Amesema kuwa serikali imejipanga vyema ili kuhakiisha kwamba inakuwa na vifaa bora na vya kisasa kwaajili ya kujifunzia na kutoa huduma za afya katika ngazi zote nchini.

"Maono ya Rais Dkt. Samia hayawezi kuwa na tija kama kutakosekana wataalamu wa kufanya kazi ndio maana nawapongeza kwa kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita kwa kuzalisha wataalamu wasaidizi katika fani Utabibu, Uuguzi, Ukunga, Famasia na wataalamu wa Maabara.

"Juhudi zenu tunazijua na tunazitambua ndugu zanguni endeleeni kuzingatia ubora maana wahitimu hawa si kwamba wanakwenda kuokoa maisha ya watu wetu bali hata sisi hapa ni wateja wao tunaomba muwapokee mtakapokuwa huko makazini"

Akijibu risala ya Mkuu wa Chuo hicho, Kipanga amesema kuwa atawasiliana na TAMISEMI pamoja na TARURA ya Mkoa wa Pwani ili kuona namna bora ya kuboresha miundombinu ya barabara ya kufika hapa chuoni na katika kampasi nyingine kama zilivyoandikwa kwenye risala.

Pia ametoa wito wa wahitimu hao kuonesha weledi katika kazi kwasababu kusoma ni jambo jingine na kufanya kazi ni jambo jingine, unaweza ukasoma lakini usielimike.

"Wito wangu kwenu ni kahakikisha yale ambayo mmeyapata mnakwenda kuyatumia pale mnapoenda kufanya kazi kwa weledi." Amesema Kipanga

Pia amewaasa kuepuka masuala ya rushwa ufisadi na kujikinga na magonjwa mbambali kwani taifa linawahitaji sana.

Aidha amesema ni muhimu mkafahamu kwamba elimu haina mwisho kimsingi wanavyosheherekea mahafali wajuae kwamba wamefungua njia ya kuendeleza taaluma waliyopata hadi wawe wataalamu bobezi katika fani zao.

Kwa Upande wa Mkuu wa Chuo, Kelvin Kenan ameiomba serikali kuwasaidia kutengeneza miundombinu ya barabara itakayofika chuoni hapo ili kuchochea maendeleo zaidi katika chuo hicho.

Kwa upande wa Wahitimu wa Chuo hicho wamewashukuru wakufunzi wao lakini pia wameomba kuwepo na bajeti za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi ili kuweza kupata elimu bora.

Pia wameiomba serikali kuwapatia mikopo wanafunzi wa vyuo vya kati kwani changamoto kubwa ni kutokuwa na fedha za kujikimu kimaisha wawapo chuoni.

Licha ya hayo wameomba kuwe na fursa ya wahitumu wa chuo hicho kwenda kusoma nje ya nchi kama ilivyo vyuo vikuu vingine.