MCHENGERWA APONGEZA KIBAHA KWA UFAULU, ATOA MAELEKEZO MAHUSUSI

July 09, 2025

Na John Mapepele

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe, Mohamed Mchengerwa ameupongeza uongozi wa Shule ya Sekondari ya Kibaha kwa kuendelea kuwa na matokeo ya ufaulu mzuri huku akiwataka kutoshuka.

Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo jana wakati alipotembelea shule hiyo na kukagua miundombinu ya madarasa, mabweni,maabara na baadaye kushuhudia wanafunzi waliokuwa wakijiunga na kuzungumza na walimu wa shule hiyo.

Waziri Mchengerwa amesema ameridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na walimu hao kwani katika kipindi chote shule imekuwa miongoni mwa shule zenye matokeo mazuri nchini.

Amesema kutokana na ongezeko la wanafunzi wa kidatu cha tano kwa mwaka huu, walimu wanatakiwa kuweka mikakati madhubuti ili kuhakikisha wanabaki katika kiwango kilekile cha ufaulu.
"Natambua safari hii tumeongeza wanafunzi wa kidato cha tano hakikisheni mnakuja na mikakati ambayo itamaintain kiwango kilekile." Amesisitiza Mhe. Mchengerwa

Kwa mujibu wa Afisa Elimu wa Mkoa wa Pwani Jimmy Daudi Nkwamu ufaulu wa kidatu cha sita mwaka huu ni asilimia 100 ambapo wanafunzi 136 kati ya wanafunzi 140 wamepata daraja la kwanza sawa na asilimia 93.7. 
Kwa upande wa matokeo ya kidatu cha nne kwa mwaka 2024 amesema wanafunzi wote 92 walipata daraja la kwanza.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amemuelekeza Afisa Elimu wa Mkoa wa Pwani kuhakikisha anafanya ziara katika wilaya zote za Mkoa huo na kubaini changamoto zote ili kuzipatia ufumbuzi.

"Ninakutaka kutoka ofisini na kwenda kwenye Wilaya zote kuona kama kuna changamoto na kutafuta ufumbuzi mara moja." Amefafanua Waziri Mchengerwa

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »