Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi wakati akiwasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) kufungua Mkutano wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika leo tarehe 15 Julai 2025.










Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akimkabidhi Madaraka Nyerere Tuzo Mahususi ya Miaka 30 ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) iliyotolewa kwa Rais wa Awamu ya Kwanza na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kutambua mchango wake katika kukuza Sekta ya Habari nchini. Tuzo hiyo imetolewa wakati wa Mkutano wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika unaofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC). Tarehe 15 Julai 2025.


……
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema wakati umefika kwa wanahabari wa Kiafrika kuonesha taswira nzuri ya Bara la Afrika kwa kuandika habari chanya zenye nguvu na za kutia moyo kuhusu Bara hili.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika unaofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC). Amesema kwa kipindi kirefu Bara la Afrika limekuwa likitegemea simulizi za vyombo vya habari vya nje ambazo zimejikita katika hatari, vita, migogoro, na kushindwa huku vikipuuza uwezo mkubwa, uthabiti, na maendeleo ya watu wa Afrika.
Amesisitiza umuhimu wa kuwa na habari zinazoonyesha ushindi wa jamii za Kiafrika, wajasiriamali wa biashara maarufu duniani, ubora wa kitaaluma wa wanafunzi wa Afrika, uvumbuzi wa vijana, ujasiri wa wanawake na michango inayoongezeka ya Afrika katika sayansi, teknolojia, utawala bora, na uchumi wa kimataifa.
Makamu wa Rais amesema ni vema kuanza kuandika historia ya Bara hili kwa maneno na sauti ya Wafrika wenyewe. Amesema Katika kuendeleza Ajenda ya 2063 ya Umoja wa Afrika, ambayo inatazamia kuwa na bara lenye amani, umoja, ustawi na heshima ya kimataifa, vyombo vya habari lazima vichukue jukumu la kuleta mabadiliko. Amesema ni lazima kutumika kama daraja linalounganisha mataifa, kuwezesha mazungumzo yenye maana katika Bara zima na kulinda utajiri wa urithi wa kihistoria na kitamaduni wa Afrika kwa vizazi vijavyo.
Pia Makamu wa Rais ametoa wito kwa washiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa Mabaraza Huru ya Habari kuandaa mapendekezo ikiwemo ya kisheria au maeneo ambayo yanahitaji kuboreshwa ili kutumia vyema manufaa ya Akili Unde (AI) katika tasnia ya habari.
Amesema zinahitajika sheria, sera na kanuni zitakazoongoza matumizi ya akili unde kwa njia ambayo inalinda maadili ya uandishi wa habari, haki ya kupata taarifa sahihi, na haki ya kutoa maoni kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Makamu wa Rais amesema licha ya faida za matumizi ya akili unde katika tasnia ya habari lakini bado zipo changamoto za usambazaji wa taarifa potoshi za makusudi ambapo vyombo vya habari Duniani vinakabiliwa na jukumu la kutofautisha taarifa sahihi na ile isiyosahihi zinazofanana.
Pia Makamu wa Rais amesema mijadala juu ya kuboresha sheria na mifumo ya udhibiti kwa vyombo vya habari na mawasiliano ni muhimu kwa kuwa vina jukumu la kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi kupitia utoaji taarifa sahihi za ukweli kuhusu nafasi za ajira na ujasiriamali, mitaji, usambazaji wa taarifa za kibiashara, na kutangaza huduma za kifedha za kidijitali. Ameongeza kwamba uwekezaji kwenye vyombo vya habari utasaidia kukuza uvumbuzi, uwajibikaji, na ushiriki wa wananchi katika shughuli za kiuchumi na kijamii.
Vilevile Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa Vyombo vya Habari Barani Afrika kuwa na sera rafiki zitakazohakikisha upatikanaji wa habari kwa makundi yote katika jamii hususani kwa watu wenye mahitaji maalum kwani ni njia bora kujenga jamii ya maarifa jumuishi.
Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa wito kwa mabaraza ya vyombo vya habari kote barani Afrika kuwa imara katika kukuza uwajibikaji wa vyombo vya habari na katika kulinda uhuru wa kujieleza. Amesema hayo ni pamoja na kushughulikia kwa wakati na kitaalamu malalamiko yote yanayowasilishwa dhidi ya vyombo vya habari na kuchukua hatua zinazofaa za kurekebisha inapobidi.
Makamu wa Rais ameongeza kwamba mabaraza ya vyombo vya habari yanapaswa kuongeza juhudi za kuimarisha uwezo wa wanahabari kwa kutoa mafunzo endelevu na fursa za kujiendeleza kitaaluma ili kukabiliana na tishio linaloongezeka la taarifa potofu za kimakusudi.
Kwa upande wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amelishukuru Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa tuzo iliyotolewa kwa Rais wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi ya kutambua mchango wake katika kukuza sekta ya habari hususani kuruhusu kuanzishwa kwa vyombo vya habari binafsi na kutoa uhuru kwa wanahabari. Amesema uamuzi huo umechangia sana katika kujenga tasnia ya habari katika Taifa.
Dkt. Mwinyi amesema tuzo hiyo itatumika kama chachu ya kuendelea kutumia vyombo vya habari kwaajili ya maendeleo ya watu wa Afrika. Aidha ameongeza kwamba hayati mzee Ali Hassan Mwinyi aliamini kwamba vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuwaunganisha wananchi na viongozi kwa kuwapa fursa ya kujieleza kujadili na kutoa maoni yao ili kwa pamoja kushiriki katika mambo muhimu yenye maslahi kwa Taifa.
Kwa upande wake Madaraka Nyerere akizungumza mara baada ya kupokea Tuzo Mahususi ya Miaka 30 ya Baraza la Habari Tanzania iliyotolewa kwa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, amesema Baba wa Taifa alitambua kwamba vyombo vya habari ni nguzo muhimu ya uhuru wa mawazo na maendeleo ya jamii.
Ameongeza kwamba wakati wa harakati za ukombozi wa kusini mwa Afrika, vyombo vya habari vilikua silaha muhimu katika kueneza ujumbe wa haki, uhuru na utu wa Muafrika. Amesema Baba wa Taifa alisisitiza kuwa uhuru wa vyombo vya habari sio anasa bali ni hitaji la msingi la jamii huru na yenye maendeleo.
Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amesema Tanzania imeendelea kushirikiana na wadau wa habari pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya habari nchini.
Amesema kupitia bajeti ya Serikali ya Mwaka 2025/2026, Serikali imeridhia kutoa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani kwenye magazeti yanayozalishwa nchini ili kupunguza gharama za magazeti hayo na hivyo kuwezesha upatikanaji wa taarifa muhimu. Pia Serikali imeendelea kutoa watalaam kwaajili ya kutoa elimu na kuhamasisha matumizi sahihi ya teknolojia katika sekta ya habari kama vile matumizi ya akili unde (AI).
Awali akitoa taarifa ya mkutano huo, Mwenyekiti wa Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika Bw. Ernest Sungura amesema changamoto zinazoikumba Tasnia ya Habari hususani Bara la Afrika zinahitaji nguvu ya pamoja katika kutafuta suluhu ya changamoto hizo, kukuza uchumi wa vyombo vya habari na kulinda uhuru wa vyombo vya habari ili viendelee kutekeleza wajibu wa kufahamisha, kufichua maovu, kuelimisha na kuburudisha kwa kuzingatia maadili na weledi.
Kauli mbiu ya mkutano huo ni “Uboreshaji wa sheria za Vyombo vya Habari na Mawasiliano ni msingi wa weledi wa uandishi wa Habari”
EmoticonEmoticon