Na Mwandishi Wetu
KAMPENI ya kitaifa ya Chuma kwa Chuma Sio yenye ya uhamasishaji wa usalama barabarani imezinduliwa rasmi leo Julai 19,2025 huku waendesha bodaboda na bajaji wakikumbushwa kuzingatia sheria za usalama barabarani ikiwa ni sehemu ya kupunguza ajali za barabarani nchini.
Akizungumza leo Julai 19,2025 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi(IGP) Camilius Wambura,Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Polisi ,Kikosi cha Usalama Barabarani ACP Joseph Mwakabonga amesema kampeni ya Chuma kwa Chuma Sio itasaidia kuwajengea uelewa zaidi madereva bodaboda na bajaji kuzingatia sheria za usalama barabarani.
"Kampeni hii ya Oryx Energies ya kutoa elimu ya usalama barabarani kwa bodaboda ni suala mtambuka ambalo kila mtu ambaye ni mtanzania anatakiwa kuwa sehemu ya kufanikisha kampeni hii ,tunawapongeza kwa kuona umuhimu wa kuwapa elimu hii ndugu zetu wa bodaboda na bajaji.
ACP Mwakabonga amesema kuwa kampeni hiyo itawafanya waendesha pikipiki na bajaji kuachana na tabia ya kutofuata sheria za usalama barabarani ,hivyo amesema ni imani yao watumiaji wa vyombo hivyo watazingatia sheria na hatimaye kupunguza au kumaliza ajali zinazotokana na pikipiki au bajaji.
Kuhusu ajali za barabarani bado imekuwa changamoto kubwa nchini hivyo kuwepo kwa wadau ambao wanaona muhimu wa kutoa elimu ya usalama barabarani ni jambo la kupongeza na kuungwa mkono.
Kuhusu vibanda vya kisasa ambavyo wamekabidhiwa na kampuni hiyo ACP Mwakabonga amesema vinakwenda kusaidia askari wa kikosi cha Usalama Barabarani kutekeleza majukumu yao vizuri kwani watakuwa katika vibanda ambavyo ni vya kisasa ambavyo vimefungwa Mfumo wa taa za sola.
“Askari polisi kwa kutumia vibanda hivi wanaweza kutekeleza majukumu yao wakati wowote kutokana na kuwa na taa ambazo zinatumia Mfumo wa sola,hivyo hata nyakati za giza kazi zetu zitaendelea.”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Energies Tanzania, Imani Mtafya, amesema kampeni hiyo inalenga kuongeza uelewa na kuchochea mabadiliko chanya kwa waendesha pikipiki na bajaji na watoa huduma wengine kuhusu usalama barabarani.
Amefafanua malengo ya Kampeni “Chuma kwa Chuma Sio Poa” ni pamoja na kutoa elimu ya usalama barabarani kwa waendeshaji bodaboda na bajaji kupitia ushirikiano na Jeshi la Polisi,kutoa michango ya vitendea kazi kama vibanda vya kisasa vya askari vinavyotumia nishati ya jua, kofia ngumu, jaketi za kuonekana usiku, vizimia moto, na vilainishi bora vya mitambo, pikipiki na magari.
Pia kupitia kampeni hiyo kampuni hiyo imetoa mafunzo ya usalama kwa wasafirishaji zaidi ya 200 kwa kila wilaya ya Dar es Salaam, huku ikilenga kupanua mafunzo haya kote nchini.
Ametoa mwito kwa wasafirishaji na watumiaji wa pikipiki kuchukua nafasi hiyo kujifunza na kuwa mabalozi wa usalama barabarani katika jamii zao. Pia alisisitiza umuhimu wa vyombo vya habari katika kueneza ujumbe huu ili kuhakikisha jamii nzima inashiriki katika kuzuia ajali.“Ajali nyingi zinaweza kuzuilika. Elimu na uwajibikaji ni silaha kubwa zaidi.”
Wakati huo huo kwa Mkurugenzi Mkuu Oryx Gas Tanzania Ltd ambayo ni moja Kati ya kampuni zilizopo chini Oryx Energies Benoit Araman amesema kampeni hiyo inalenga kuelimisha na kuhamasisha usalama wa barabarani, hasa kwa waendeshaji wa pikipiki na bajaji, ambao ni sehemu muhimu ya usafiri wa kila siku.
“Tunaamini kwa pamoja tunaweza kupunguza ajali, kulinda maisha, kutumia nishati safi na kusaidia uchumi na maendeleo ya taifa letu,”amesema Araman na kusisitiza kampeni hiyo wanashirikiana na Jeshi la Polisi kutoa elimu ya usalama barabarani, pia wamekabidhi vibanda vya kisasa vya askari wa usalama barabarani vinavyoendeshwa kwa nishati ya jua.
Pamoja na hayo amesema Oryx Energies pia imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na kutekeleza maagizo ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo tangu Julai 2021 wamekuwa wakitekeleza mkakati huo lengo likiwa kuhakikisha Watanzania wanatumia nishatisafi.
Awali Mwenyekiti wa Chama cha bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam na Taifa Said Chega amesema ni muhimu kuendelea kupata elimu ya usalama barabarani na kusisitiza kupitia kampeni ya Chuma kwa Chuma Sio poa watapunguza ajali za barabarani kwani watakuwa wanakumbushwa kuzingatia sheria za usalama barabarani.
“Kila siku katika shughuli zetu tunapokea madereva wapya wapo wa elimu ya msingi na Sekondari ambao wanakuja kuungana nasi hivyo kunapokuwa na mafunzo ya aina hii yanasaidia kutujengea uelewa na kuchukua tahadhari kwa kuheshimu sheria za usalama barabarani.
Amesisitiza kuwa kuna haja ya waendesha pikipiki kuendelea kupatiwa elimu kwani ndio wanasafirisha abiria kila siku hivyo wanapokuwa na elimu hiyo maana hata abiria nao wanakuwa salama."Tunawapongeza Oryx Energies kwa kampeni hii lakini pia tunawapongeza Jeshi la Polisi kwa kuwa mstari wa mbele kutupatia mafunzo kama haya Mara kwa mara.
EmoticonEmoticon