WMA YAENDESHA ZOEZI LA UHAKIKI MITA ZA UMEME VIWANDANI

June 19, 2025

 



Wakala wa Vipimo (WMA) unaendesha zoezi la kuhakiki mita za umeme zilizofungwa katika viwanda mbalimbali nchini ili kuhakikisha Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) inapata mapato stahiki na wenye viwanda wanalipa gharama stahiki kulingana na huduma ya umeme wanaotumia.

Hayo yalibainishwa Juni 18, 2025 na Meneja wa WMA Makao Makuu, Albogast Kajungu wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika uwanja wa Chinangali, Dodoma.

Kajungu alisema kuwa hadi sasa WMA imekagua mita za umeme zaidi ya 2,000 huku lengo likiwa ni kuhakiki mita zote zilizo kwenye matumizi katika viwanda vyote nchini katika zoezi lililoanza Mei mwaka huu



“Hali inaonesha kwamba mita nyingi zilizo kwenye matumizi viwandani ziko vizuri. Chache ambazo tumekuta zina mapungufu, tumewasiliana na Mamlaka husika kwa ajili ya kuzirekebisha na nyingine kuzibadilisha ili kuhakikisha vipimo viko sahihi kwenye eneo hilo,” alisema Kajungu.
Akieleza zaidi, alisema kuwa zoezi hilo la uhakiki linahusisha mita zote za umeme zilizo katika matumizi lakini Wakala imeona ianze na zile zilizoko viwandani kwakuwa zinatumia umeme mkubwa hivyo ikiwa haziko sawasawa, kuna uwezekano wa TANESCO au wenye viwanda kupata hasara.

Aidha, alieleza kuwa zoezi la uhakiki linahusisha pia bidhaa za chuma hususan zinazotumika katika ujenzi kwani kumekuwa na malalamiko katika eneo hilo.

Akifafanua, Kajungu alisema kuwa sekta ya ujenzi hapa nchini inakua kwa kasi ambapo miradi mingi ya ujenzi inayotekelezwa na serikali inatumia bidhaa za chuma hivyo WMA imeona iongeze nguvu kuhakiki bidhaa hizo hususani zinazozalishwa kwenye viwanda vya ndani ili kuhakikisha zina vipimo vilivyo sahihi.




Alisema kuwa wazalishaji wanajitahidi kuzalisha kwa kuzingatia viwango lakini lengo la Wakala hiyo ni kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi zinaendelea kuwa na vipimo sahihi ili kuwalinda wananchi dhidi ya madhara ambayo yanaweza kutokea kwa kutumia bidhaa za chuma ambazo hazikidhi vipimo vinavyokubalika kisheria.

Sambamba na uhakiki wa mita za umeme na bidhaa za chuma, Kajungu alieleza kuwa zoezi hilo la uhakiki pia linahusisha dira za maji zilizo kwenye matumizi kwakuwa ndizo zenye malalamiko yanayohusiana na bili na mengineyo.

Hata hivyo, alibainisha kuwa pamoja na kuhakiki bidhaa zilizo kwenye matumizi, WMA kupitia Kituo cha Vipimo Misugusugu kilichopo mkoani Pwani, pamoja na kazi nyingine, huhakiki mita mpya za umeme na dira mpya za maji ili zinapokwenda kufungwa kwa wateja ziwe zimeshathibitishwa kuwa vipimo vyake ni sahihi.

Kajungu alitumia fursa hiyo kuwaalika wananchi wafike kwa wingi kwenye Banda la Wakala wa Vipimo ili kujipatia elimu kuhusiana na vipimo mbalimbali vinavyotumika ili kuwalinda kwa maana ya kupata thamani ya fedha wanazotoa wanapokwenda kununua bidhaa.

Wakala wa Vipimo ni mojawapo ya Wakala za Serikali yenye dhima ya kutoa huduma za kumlinda mlaji kupitia uhakiki wa vipimo, usimamizi wa vipimo na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Majukumu yake ni kumlinda mlaji na umma kwa ujumla kupitia uhakiki na uthibiti wa vipimo vinavyotumika katika biashara na huduma nyingine ili kuhakikisha kuwa vipimo hivyo ni sahihi na vinatumika kwa usahihi kulingana na Sheria ya Vipimo Sura 340, mapitio ya mwaka 2002 na maboresho yake ya mwaka 2026 pamoja na kanuni zake.




Share this

Related Posts

Previous
Next Post »