MADIWANI WA JIJI LA TANGA WATEMBELEA SOKO KUU LA NAFAKA TANDALE

May 13, 2025


Kinondoni. Mei 12, 2025.


Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Tanga wameianza ziara yao ya siku tatu katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa kikao kifupi na uongozi wa Manispaa hiyo, ukiongozwa na Mstahiki Meya Mhe. Songoro Mnyonge, na kufuatiwa na ziara ya kutembelea soko kubwa la nafaka la Tandale lililopo katika Manispaa hiyo.

Katika salamu zake kwa wageni wake, Mstahiki Songoro amesisitiza umuhimu wa Halmashauri kujitegemea kwa kukusanya mapato ili kuweza kupanga na kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati bila kusubiri kuletewa fedha na wahisani au serikali kuu.

Amesema Kinondoni ni mji unaoendelea kukua ukiwa na wakazi zaidi ya milioni moja, na makusanyo ya mapato kwa mwezi yakiwa ni zaidi ya shillingi Billion tano, ambayo yanawezesha Halmashauri hiyo kuanzisha miradi mikubwa itakayowapatia mapato, akitolea mfano wa uwanja wa mpira wa miguu wa Halmashauri hiyo ambao huingiza kiasi cha shillingi millioni sita kwa mchezo mmoja wa timu za Simba au Yanga, huku uwanja huo ukiwa na maduka 72 ambapo kila moja hulipa kodi ya pango ya kati ya shillingi laki tano hadi sita kwa mwezi.

Wakiwa katika soko la Tandale, Afisa Masoko wa Manispaa ya Kinondoni, Goodlucky Kabage aliwaeleza Waheshimiwa Madiwani kuwa, soko hilo lililoanza kabla ya uhuru, limejengwa upya kuanzia mwaka 2018 na kukamilika Septemba 2024, likiwa na sakafu (ghorofa) tatu na eneo la chini (basement) kwa gharama ya shillingi Billion 10.2, likiwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 2000, na kwasasa lina wafanyabiashara 1075 wa bidhaa tofauti.

Mbunge wa Tanga Mjini, Mhe. Ummy Mwalimu aliungana na madiwani wenzake katika ziara hiyo iliyoongozwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Mhe. Abdulrahman Shiloow.



Share this

Related Posts

Previous
Next Post »

EmoticonEmoticon

:)
:(
=(
^_^
:D
=D
=)D
|o|
@@,
;)
:-bd
:-d
:p
:ng