Na Hadija Bagasha Tanga,
Mkazi wa Kwasemangube Wilayani Korogwe Mkoani Tanga Jane Athumani Pochi ameangua kilio baada ya kurejeshewa eneo lake la kilimo alilopokonywa kwa kipindi cha miaka mitatu.
Tjmu ya kampeni ya msaada wa Kisheria (Legal Aid) ya Rais Dkt Samia Suluhu Hasaan imefanikiwa kumaliza mgogoro huo wa muda mrefu wa shamba la ekari mbili kati ya Jane Athuman na Willium Michael uliodumu kwa kipindi cha miaka mitatu.
Mgogoro huo ulianza baada ya mume wa mama huyo kumuuzia ekari moja bwana Willium Michael ambapo baadae tena aliendelea kumega eneo la shamba hilo na kumuongezea Willium bila kumshirikisha mke wake na hatimaye kuifanya familia hiyo ikose mahala pa kufanyia shughuli za kilimo kwa kipindi hicho.
Timu hiyo imekutanisha pande mbili hizo kati ya muuzaji na mnununuzi pamoja na mke wa muuzaji ambapo mgogoro huo ulifanyiwa usuluhishi huku pande mbili hizo zikiridhia kila mmoja kubaki na umiliki wa ekari moja moja.
Akizungumza huku akimwaga machozi mama huyo amesema anamshukuru Rais Dkt Samia kwa kuwaletea kampeni hiyo ambayo imekuwa mkombozi hususani kwa wananchi wanyonge.
"Ninamshukuru sana Rais Dkt Samia kwamaana mume wangu aliuza eneo bila kunishirikisha mimi lakini kupitia kampeni hii imeweza kutupatanisha nimeweza kurejeshewa eneo langu ninashukuru kwa maana sasa tumeshagawana kila mtu heka yake tutakuwa tunaishi kwa amani na mama Samia Mungu akubariki, "alisisitiza Jane.
Kwa upande wake Willium Michael ambaye ndiye aliyeuziwa eneo hilo amesema kwamba suala hilo limeshakwisha kwa kuwa tayari sasa wamekwisha gawana eneo hilo la ekari mbili kila mtu kumiliki ekari moja moja.
"Watu tuwe makini kwanza unapouziwa kitu uhakikishe kabisa kwamba huyo mtu anayekuuzia je hiyo mali ni yakwakwe na kama ni ya familia je imeshirikisha watu wengine wa ndani ya familia kwahiyo hili ni jambo ambalo limetufunza, "alibainisha Willium.
Wakili George Banoba kutoka Wizara ya Katiba na Sheria baada ya kusuluhisha mgogoro huo amesema kama timu ya msaada wa kisheria anamshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuleta kampeni hiyo kwani katika maeneo mengi mengi waliyopita wamegundua wananchi wengi wana changamoto na hawapati majawabu ya changamoto zao.
"Tukiwa siku ya sita ya utekelezaji wa kampeni ya Mama Samia katika Hlamashauri ya Korogwe mji tunaandika historia nyingine ya mafanikio ambapo baada ya kuetembelea kata ya pili tulikutana na changamoto ya bwana mmoja aliyenunua eneo kutoka kwa baba wa familia moja ambaye hakumshirikisha mke wake kwenye uuzaji lakini leo baada ya kufika tumewakutanisha pande zote mbili wameweza kuridhiana na kusuluhishana, "alisisitiza Wakili Banoba.
Mwisho.
EmoticonEmoticon