
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa Meneja wa Gesi Asilia wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Dkt. Esebi Nyari kuhusu namna ya matumizi ya gesi katika vyombo vya moto wakati wa kukagua mabanda ya maonesho katika Mkutano wa 11 wa Petroli wa Afrika Mashariki unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC). Tarehe 05 Machi 2025.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati akiwasili katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam kwaajili ya Ufunguzi wa Mkutano wa 11 wa Petroli wa Afrika Mashariki leo tarehe 05 Machi 2025.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa 11 wa Petroli wa Afrika Mashariki unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam. Tarehe 05 Machi 2025.




MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito wa kuimarishwa ushirikiano zaidi kwa Mataifa ya Afrika Mashariki ili kuweza kunufaika na sekta ya nishati ambayo inaendelea kukua kwa kasi.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akifungua Mkutano wa 11 wa Petroli wa Afrika Mashariki unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam. Amesema ni muhimu kuungana pamoja kuweza kutumia rasilimali iliyopo katika sekta ya nishati Afrika Mashariki na kutengeneza njia ya maendeleo endelevu na ustawi wa kudumu wa ukanda huo. Pia amewakaribisha wawekezaji na wadau wa maendeleo kuungana na Mataifa ya Afrika Mashariki katika kuendeleza sekta hiyo.
Makamu wa Rais amehimiza majadiliano katika Mkutano huo yaweze kusaidia katika sera za mataifa husika kwa maendeleo endelevu ya sekta ya nishati. Amesema ni lazima kuendelea kuhamasisha uhamaji wa haki kuelekea katika matumizi ya nishati safi na kuhakikisha athari za kiuchumi na kijamii za mabadiliko hayo zinakuwa sawa kwa watu wote na kila mmoja ananufaika na mabadiliko kuelekea matumizi ya nishati safi bila kuachwa nyuma.
Makamu wa Rais amesema ni muhimu kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutumia kwa ufanisi rasilimali zote za nishati ikiwemo mafuta ili kuweza kukabiliana na upungufu wa nishati kutokana na kuongeza kwa mahitaji hayo katika kufikia maendeleo kwa haraka. Ameongeza kwamba rasilimali za nishati zitaweza kuwa chanzo kikuu cha mapato kwa serikali na hivyo kusaidia katika uwekezaji kwenye miundombinu na huduma za kijamii na kuunga mkono ajenda nzima ya maendeleo.
Amesema Afrika Mashariki imejaaliwa rasilimali kubwa ya nishati ikiwemo mafuta huku mataifa yakiwa na ugunduzi mbalimbali kama vile kugunduliwa kwa gesi asilia nchini Tanzania, mafuta nchini Uganda, Kenya na Sudan, Methane kwa nchi ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na nishati ya jotoardhi kwa nchi za Tanzania na Kenya.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema maendeleo ya teknolojia ni fursa kwa nchi zinazoendelea kuongeza uwezo wa uvunaji endelevu wa nishati ya mafuta. Ameongeza kwamba ili na maendeleo endelevu ya sekta ya nishati ni muhimu mapato yanayotokana na uwekezaji huo yaweze kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo, kutengeneza ajira na uwekezaji katika jitihada za kurejesha mazingira yaliyoharibiwa. Amesema ni vema sera na sheria kujumuisha utengaji wa asilimia kadhaa ya mapato yatokanayo na rasilimali ya mafuta kwaajili ya matumizi ya baadae.
Kwa upande wake Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za kuendeleza mkondo wa juu kwa lengo la kugundua na kuendeleza vyanzo vya gesi hapa nchini. Amesema katika uongozi wake kwa upande wa mkondo wa juu hatua muhimu imefikiwa ikiwemo kuimarisha uzalisha wa gesi asilia katika vitalu ya Songosongo na Mnazi bay ambavyo kimsingi ni maendeleo kwenye uchumi wa gesi.
Aidha Dkt. Biteko ameongeza kwamba maendeleo mengine ni pamoja na kuongezeka kwa ushiriki wa kampuni ya Serikali ya TPDC katika kitalu cha Mnazi bay kutoka ushiriki wa asilimia 20 hadi asilimia 40.
EmoticonEmoticon