NA WILLIUM PAUL, MWANGA.
WAJUMBE wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeridhishwa na ubora wa mradi wa maji Same Mwanga Korogwe ambao umegharimu zaidi ya Bilioni 400 na kudai kuwa thamani ya fedha inaonekana katika mradi huo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Augustine Vuma mara baada ya kutembelea mradi huo ambapo alisema kuwa, hali ya upatikanaji wa maji kwa sasa katika miji ya Mwanga na Same ni ya kuridhisha kwani wananchi wanapa maji kwa masaa 24.
“Kamati imeridhishwa na ubora wa mradi pamoja na upatikanaji wa maji kwa sasa hivyo kamati inaipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongpzwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kujenga mradi huo na zimetolewa kwa wakati” alisema Vuma.
Alisema kuwa, jukumu la sasa kwa Wizara ya maji kupitia mamlaka yake ya Mwanga Same ni kutunza mradi huo kwa kushirikiana na Wananchi ili uendelea kuwa bora na kudumu muda mrefu ili kuhakikisha kuwa wananchi hawarudi kule walipotokea kukosa maji au kupata kwa mgao.
Aidha wameiagiza mamlaka hiyokuhakikisha inatekeleza mpango wa usambazaji maji kikamilifu katika maeneo ya mamlaka ili kuwafikiwa wahitija na kutimiza adhima ya Serikali ya kuwafikia wananchi wengi huduma.
Alisema kuwa, mamlaka hiyo inatekeleza mpango wa ulinzi wa vyanzo vya maji na miundombinu yake pamoja na kuweka mpango wa muda mfupi na mrefu wa ukarabati wa miundombinu ya maji ili kuhakikisha mradi unaendeshwa kwa ufanisi na katika hali ya uendelevu ambapo jambo hilo litapelekea mradi huo kutoa tija.
“Mamlaka ya maji Same Mwanga hakikisheni mnaimarisha mkakati wenu wa ushirikiano wa kibiashara na wadau mbalimbali wakiwemo wateja wakubwa ili kuweza kuwafikia kihuduma jambo ambalo litawezesha kuongeza wigo wa kiwango cha ukusanyaji wa mapato pamoja na kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kulipia Ankara za maji kikamilifu na kwa wakati ili kuepuka changamoto za madeni ambayo imekuwa kikwazo kwa mamlaka nyingi nchini” alisema Vuma.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa mamlaka ya Maji Same Mwanga (SAMWASA), Mhandisi Rashid Mwinjuma alisema kuwa, kupitia mradi huo kwa sasa wananchi wa Mwanga na Same wanapata maji ya uhakika masaa 24, ambapo hali hiyo imesaidia mapato yameongezeka kutoka milioni 40 kwa mwezi hadi kufikia milioni 70.
Mhandisi Mwinjuma alisema kuwa, hata wateja wameongezeka kutoka 4000 hadi kufikia 6000 huku akidai kuwa mwamko wa wananchi kuomba kuunganishiwa huduma ya maji umekuwa mkubwa.
“Kwa sasa tunajukumu la kuendelea kusambaza mtandao wa maji ili kuwafikia wateja wengi ili kusaidia kukusanya fedha za kuweza kuendeshea mradi huu na kwa siku tumekuwa tukipokea wastani wa watu 50 wanaotaka kuunganishiwa na huduma ya maji lakini tumeendelea kutoa elimu ili watambue umuhimu wa kulipia Ankara zao kwa wakati” alisema Mhandisi Mwinjuma.
EmoticonEmoticon