📌 *Wazungumzia jinsi Mfuko wa Uwekezaji Denrmark (IFU) utakavyosaidia kuendeleza Sekta ya Nishati nchini*
📌 *Dkt. Kazungu akaribisha uwekezaji Rumakali, Ruhudji na miradi iliyopo katika Mpango Mahsusi wa Taifa wa Nishati (2025-2030)*
📌 *Denmark yaahidi kuendeleza ushirikiano*
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Khatibu Kazungu amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mhe. Jesper Kammersgaard na Makamu wa Rais wa Mfuko wa Uwekezaji wa Serikali ya Denmark (IFU) Bw. Theo Ib Larsen.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Jijini Dodoma tarehe 27 Machi, 2025, Mhe. Kammersgaard pamoja na Larsen walikuwa na lengo la kueleza kuhusu Mfuko wa Uwekezaji wa Serikali ya Denmark ulioanzishwa mwaka 1967 ili kusaidia maendeleo katika nchi zinazoendelea kwa kutoa mitaji kwa kampuni zinazotaka kuwekeza katika masoko yanayoibukia barani Afrika, Asia, Amerika ya Kusini na sehemu za Ulaya.
Viongozi hao wameeleza kuwa IFU inaweza kutoa msaada wa kifedha na kiufundi katika eneo la Nishati Jadidifu hasa upepo na umeme jua na kusaidia katika masuala ya athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Aidha wameeleza kuwa mfuko wa IFU unasaidia katika eneo la uzalishaji wa umeme jadidifu, usafrishaji na usambazaji wa umeme.
Katika kikao hicho, Balozi Kammersgaard ameahidi kushirikiana na Wizara ya Nishati katika kusaidia miradi yenye matokeo makubwa kama vile usafirishaji wa umeme kutoka katika Mradi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere, na kuangalia uwezekano wa uwekezaji katika miradi ya jotoardhi hasa katika eneo la upembuzi yakinifu na uchorongaji.
Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Kazungu kwa upande wake, alimshukuru Balozi na Timu yake kwa kuamua kuitembelea Wizara ya Nishati na kuelezea kwamba Denmark ina ushirikiano wa muda mrefu na Tanzania hasa katika nyanja za Elimu na Afya.
Ameeleza kuwa sasa ni wakati muafaka wa kuongeza ushirikiano katika nyanja ya Nishati ambapo ameikaribisha IFU kuwekeza katika miradi ya uzalishaji umeme ya Ruhudji (MW 358) na Rumakali (MW 222) ambayo Wizara imeshakamilisha maandalizi muhimu ikiwemo ya upembuzi yakinifu.
Aidha ametoa wito kwa IFU kusaidia kuongeza vyanzo vinavyotokana na umeme jadidifu nchini kama ilivyoainishwa katika Mpango Kabambe wa Kuendeleza Sekta ya Nishat Nchini (PSMP, vyanzo hivyo ni pamoja na vitokanavyo na maji, upepo na jotoardhi.
Vilevile ameiomba IFU kwa kushirikiana na Serikali ya Denmark kuona namna ya kusaidia utekelezaji wa Mpango Mahsusi wa Taifa wa Nishati wa 2025 – 2030 uliozinduliwa Mwezi Januari, 2025 ambao unalenga kuendeleza vyanzo vya uzalishaji wa umeme kupitia nishati jadidifu na kuongeza kiwango cha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Maazimio yaliyofikiwa katika kikao hicho ni kuundwa kwa timu ya pamoja ya wataalam kutoka Wizara ya Nishati na IFU ambayo itafanya kazi ya kupitia maeneo mbalimbali yatakayopendekezwa, kuchambuliwa na hatimaye kufikishwa kwa ngazi za juu za Wizara na IFU kwa hatua zaidi.
EmoticonEmoticon