
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amewataka Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji kutekeleza majukumu yao kwa uzalendo, uadilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa ambavyo vinaweza kupelekea uingiaji wa wahamiaji haramu nchini.
Bashungwa ameeleza hayo, leo Machi 04, 2025 katika kikao kazi na Maafisa na Askari wa Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uokoaji, Idara ya Uhamiaji na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) katika wilaya ya Karagwe, Mkoa wa Kagera.
“Wizara itawasimamia kikamilifu maafisa Uhamiaji katika kutekeleza majukumu yao. Wale ambao watakosa uzalendo na uadilifu, na kuwa sehemu ya chanzo cha kuchochea uingiaji wa wahamiaji haramu kwa lengo la kujipatia fedha au rushwa, tutawachukulia hatua kali za kisheria na za kiutumishi” amesema Bashungwa
Bashungwa amesema Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa Mikoa ambayo iko mipakani, ambao umekuwa ukikumbwa na changamoto ya baadhi ya wageni kutoka nchi jirani kuingia kinyume na taratibu kutokana na ukubwa wa mpaka.
Aidha, Bashungwa ametoa wito kwa viongozi wa vijiji na kata, kuwa mstari wa mbele kusimamia ili kukomesha suala la uhamiaji haramu bila kumuonea au kumkomoa mtu kwa kutoa taarifa kwa maafisa wa uhamiaji pale zinapohitajika.
Amewahimiza wananchi kutoa taarifa pindi watakapoona Askari wa Idara ya Uhamiaji anafanya vitendo ambavyo ni kinyume na maadili, sheria na taaluma yake ili kuhakikisha kila mgeni anayeingia nchini anaingia kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Julius Laiser ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuviwezesha Vyombo vya Ulinzi na Usalama ikiwemo Idara ya Uhamiaji Wilaya ya Karagwe kupewa gari jipya.




EmoticonEmoticon