Na Mwandishi Wetu
MENEJA Masoko na Mauzo wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Shaban Fundi amesema ili kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034 kuna hitaji kubwa la kutoa elimu kuhusu nishati hiyo ili wananchi wawe na uelewa wa kutosha na kuitumia.
Ameyasema hayo alipokuwa akishiriki mjadala wa jopo kuhusu mipango na mikakati ya nishati safi ya kupikia wakati wa Kongamano la 11 la Petroli la Afrika Mashariki na Maonyesho 2025.
Akitoa maoni yake amefafanua pamoja na changamoto katika usambazaji wa nishati safi, hususan LPG, kuna hitaji kubwa la elimu juu ya mpito wa nishati ili kufikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania kuhamia nishati safi ifikapo mwaka 2034.
“Kuna haja kwa wadau wa nishati safi kushirikiana na Serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu nishati, wapo ambao wanaamini kupika kwa kuni au mkaa chakula ndio kinakuwa kitamu…
“Pia wapo wanaoamini kupika kwa gesi kuna madhara .Hivyo tunalojukumu la kutoa elimu na hatimaye wananchi waone nishati safi ya kupikia ndio suluhisho sahihi katika kupika.”
Pia amesema kwa sasa hali ilivyo watumiaji wengi wa mkaa wako mijini, sio vijijini; kwa hivyo, juhudi za serikali lazima pia zizingatie eneo hilo katika mpito wa nishati.
“LPG ni nafuu kuliko mkaa kwa kiwango sawa cha matumizi.Kwa kutambua juhudi na msaada wa serikali kupitia REA na wadau wengine, tufikirie kutoa ruzuku sio tu mitungi ya gesi bali pia kujaza gesi kwa watu wa kipato cha chini hasa vijijini,”amesema Fundi.
Kuhusu Oryx Gas amesema kwa nafasi yao wamefanya kazi ya kutoa elimu kwa wananchi kuona umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia ambayo mbali ya kutunza mazingira pia inasaidia kujikinga na madhara ya kiafya yanayotokana na chembechembe za moshi wa kuni au mkaa.
Pia amesema katika kufikisha gesi ya kupikia maeneo ya vijijini wameendelea kuongeza vituo vya kusambaza gesi kupitia Mawakala wao walioko katika Wilaya na Vijiji huku akitoa rai kwa wadau wengine kupeleka gesi vijijini kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wake.
Meneja Masoko na Mauzo wa Oryx Gas Shaban Fundi akitoa maoni yake alipokuwa akichangia hoja katika kongamano la 11 la Petroli la Afrika Mashariki na Maonesho ya 25 yanayoendelea Jijini Dar es Salaam .
EmoticonEmoticon