WAKURUGENZI WA UFUATILIAJI NA TATHMINI NGAZI YA WIZARA WAKUTANA KUPITIA TAARIFA YA UTENDAJI WA SERIKALI

February 12, 2025


Na Mwandishi wetu - Iringa.

Wakurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini ngazi ya wizara wamekutana leo tarehe 12 Februari 2025 katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa  lengo la kupitia Taarifa ya Utendaji wa Serikali (Government Performance Report kwa Mwaka wa Fedha 2023/24). 





Kikao kazi cha wakurugenzi hao kimeandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu na kuhudhuriwa na Wakurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini na Maafisa kutoka katika Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini ndani ya wizara.

Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. James Henry Kilabuko, Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini ya  Utendaji wa  Serikali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Sakina Mwinyimkuu amesema, jukumu la Ufuatiliaji na Tathmini ni muhimu katika kuboresha utendaji wa serikali kwa ujumla hivyo  Serikali imeendelea kutoa msukumo na kuboresha Miundo na Mifumo kwa kuandaa Miongozo ya Ufuatiliaji na Tathmini Ili kuimarisha U&T ndani ya Serikali. 



“Dhumuni kubwa ni kuboresha utendaji wa Serikali na utoaji huduma bora kwa wananchi hivyo wataalam wa Vitengo mnapaswa kusimamia  na kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo yaliyoainishwa katika mipango ya  serikali” amebainisha Bi. Sakina 

Aidha, Bi. Sakina amewaasa wataalam kutofanya kazi kwa mazoea, uoga au kutojiamini, kwani kwa kufanya hivyo serikali haitafikia malengo na kupunguza umuhimu wa kuanzisha Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini. Hivyo ni vema kuifanya ufuatiliaji na tathmini kuwa nyenzo ya msingi ya kusaidia utendaji wa taasisi, sekta na nchi kwa ujumla.

Kikao kazi hicho pamoja na  mafunzo ya namna ya matumizi ya  Miongozo ya Ufuatiliaji na Tathmini (U&T) katika taasisi za serikali iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu kitafanyika kwa siku mbili kuanzia leo tarehe 12 hadi 13 februari 2025.






Share this

Related Posts

Previous
Next Post »