DKT.BITEKO AONGOZA HARAMBEE UJENZI WA KANISA KUU JIMBO LA RULENGE-NGARA

February 23, 2025


📌 *Ampongeza Mhashamu Severine Niwemugizi kwa maono ya kujenga Kanisa*


📌 *Rais Samia apongezwa kwa ushirikiano wake na taasisi za dini*


*Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati*


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amempongeza  Askofu wa Jimbo Katoliki Rulenge -Ngara, Mhashamu Severine  Niwemugizi kwa maono ya kujenga  Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Rulenge -  Ngara mkoani Kagera.


Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo Februari 22, 2025 jijini Dar es salaam wakati aliposhiriki katika harambee ya ujenzi wa Kanisa hilo.


“ Nakupongeza baba Askofu kwa kuwa na maono makubwa ya kujenga hekalu la bwana la viwango vya juu na kuwaza makubwa,” amesema Dkt. Biteko.

Ameendelea “ Binafsi namuona Baba Askofu kama mbeba maono wa Jimbo na sisi tumshike mkoni ili nia yake iweze kufanikiwa. Kiu hiyo itafanikiwa kwa kuwa nia ipo na kanisa litajengwa na sisi wenyewe,” 


Aidha, Dkt. Biteko amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa kumpa fursa ya kumwakilisha kushiriki katika tukio hilo la harambee ya ujenzi wa kanisa.

Askofu wa Jimbo Katoliki Rulenge -Ngara, Mhashamu Severine  Niwemugizi  amesema kuwa Jimbo hilo liliundwa mwaka 1960 na kwa sasa linajumuisha Wilaya za Biharamulo, Chato na Ngara. 


Ameongeza kuwa Kanisa lililopo lilianza kama kigango na limekuwa likipanuliwa mara kwa mara kulingana na mahitaji.


Ameendelea kwa kusema kuwa wamefikia uamuzi wa kujenga  kanisa jipya ili kukidhi mahitaji ya sasa.

Awali akizungumza wakati wa misa takatifu, Askofu Niwemugizi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kuwasaidia kufanya harambee kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Rulenge -Ngara mkoani Kagera na kuwa hatua hiyo inadhihirisha upendo upendo wa dhati wa Rais kwa wananchi wa Ngara na Watanzania kwa ujumla.


“ Katika kujenga nyumba ya bwana tulipopiga hodi kwa Mhe. Rais Samia kumuomba atusaidie kujenga nyumba ya heshima ya bwana alikubali na tunafurahi jioni hii amemtuma Dkt. Biteko awe nasi, tumtukuze Mungu katika ushirikiano huu anaouweka na kwamba viongozi wa Serikali wako tayari kusaidia watu katika kutimiza nia zao,” amesema Askofu Niwemugizi.

Mhandisi wa mradi wa ujenzi wa Kanisa hilo, Daudi Masaka amesema kuwa ujenzi wa kanisa hilo hadi kukamilika kwake utagharimu jumla 

ya shilingi bilioni 7,700,000/=


Aidha, ametaja baadhi ya sehemu ya kanisa hilo kuwa sakafu ya pili ya jengo litakuwa na uwezo wa kubeba watu 2100, makanisa madogo mawili na sehemu ya makaburi manne.



Aidha, harambee hiyo imehudhuriwa pia na  viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Fedha, Mhe. Mwigulu Nchemba.


MWISHO

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »