DKT. KIKWETE AONGOZA WAJUMBE WA MKUTANO MKUU WA CCM KUSAFIRI KWA TRENI YA SGR KWENDA DODOMA

January 16, 2025


Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (katikati) na Mkewe Salma Kikwete (kulia) wakielekea kupanda Treni ya Mwendo kasi ya SGR wakati wakielekea Jijini Dodoma kushiriki Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao utafanyika Januari 18 hadi 19, 2025. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa.

...........................................

Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam

WAJUMBE 600 wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiongozwa na Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete wametia fora kwa kusafiri na treni ya Mwendo kasi ya SGR kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Dodoma kushiriki mkutano huo utakaoanza Januari 18 na 19, 2025.

Hali hiyo imeonekana leo asubuhi Januari 15, 2025 katika Stesheni ya Treni ya Magufuli Dar es Salaam ambapo kuanzia saa 12 hadi saa 2: 30 asubuhi wajumbe hao makundi kwa makundi walifika katika stesheni hiyo na saa 3: 30 waliondoka kwa treni maalumu  kuelekea jijini Dodoma.

Mbali ya wajumbe hao watu wengine walioondoka na treni hiyo kwenda kwenye mkutano huo ni wasanii mbalimbali wakiongozwa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao, Steve Nyerere na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali,

 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa tukio hilo alisema jumla ya wajumbe 600 watasafiri kwa usafiri huo wa treni hiyo pamoja na wattu wengine jumla yao itakuwa ni 900.

“ Shirika letu limepewa heshima kubwa ya kuwasafirisha wajumbe hawa kwani wangeweza kusafiri kwa ndege, mabasi na magari yao binafsi lakini kazi hiyo tumepewa sisi,” alisema Kadogosa.

Alisema kwao kusafirisha wajumbe hao sio mara ya kwanza kwani walishawahi kusafirisha wajumbe kutoka mikoa ya kanda ya ziwa  na kuwa kwa kuaminiwa huko na kutumi usafiri wao kwao ni fursa kibiashara.

Alisema wajumbe ambao watatumia treni hiyo kusafiri kwenda Dodoma ni kutoka Zanzibar, Mtwara, Lindi, Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani.

“ Treni hii maalumu kwa ajili ya kusafirisha wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM haitaathiri  ratiba za safari za treni za kila siku ambazo zitaendelea kama kawaida,” alisema Kadogosa. 

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu safari hiyo ya wajumbe hao kuelekea Dodoma.
Baadhi ya waandishi wa habari ambao waliambatana na wajumbe hao kwenda Dodoma wakizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa kabla ya kuanza kwa safari hiyo.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao, Steve Nyerere akijadiliana jambo na wenzake Stesheni ya Treni ya Magufuli kabla ya kuanza safari ya kwenda Dodoma kushiriki mkutano huo.

Muonekano wa Treni Maalumu ya SGR ambayo inawabeba wajumbe hao wa mkutano mkuu wa CCM.
Baadhi ya wajumbe hao na abiria wengine wakisubiri kuondoka kuelekea Dodoma.
Wahudumu wa Treni ya SGR wakiwa tayari kwa safari ya kuelekea Dodoma na wajumbe hao.
 

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »