MILIONI 390 KUSAMBAZA MAJIKO YA GESI 19,530 KWA BEI YA RUZUKU MKOANI MARA

December 03, 2024
-Kila Wilaya kupata majiko 3,255

-RC Mara ahamasisha wananchi kuchangamkia fursa

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatarajia kusambaza majiko ya gesi (LPG) ya kilo 6 yapatayo 19,530 Mkoani Mara ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa Mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034.

Hayo yamebainishwa Desemba 2,2024 na Mhandisi Mwandamizi wa Wakala wa Nishati Vijijini(REA),Deusdedith Malulu ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi.

"REA ni mdau mkubwa wa kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na kwa awamu hii tumekuja na mradi huu wa majiko ya gesi," amesema Mha. Malulu.

Amesema kwa awamu hii REA itasambaza jumla ya majiko ya gesi ya kilo sita 452,000 nchi nzima kwa gharama ya shilingi bilioni 8.6.

Aidha, Mha. Malulu alizungumzia miradi mbalimbali inayoratibiwa na wakala ikiwemo uuzwaji wa sola za majumbani kwa bei ya ruzuku ya hadi 75% pamoja na uwezeshwaji wa ujenzi wa vituo vya bidhaa za mafuta ya petroli na dizeli kwa maeneo ya vijijini.

Akizungumzia kuhusiana na fursa hizo za REA, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi amewahamasisha wananchi kuchangamkia fursa hizo ili kujiletea maendeleo, kuimarisha afya zao sanjari na kuhifadhi mazingira.

"Natoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa zilizotangazwa na REA, vijana mjitokeze kwa wingi hususan waendesha bodaboda maeneo ya vijijini mjipange kuomba mkopo mfungue vituo vya mafuta hasa ikizingatiwa wateja wakubwa wa mafuta vijijini ni boda boda," alisisitiza Mhe.Kanali Mtambi.

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unaendelea na utekelezaji wa mkakati wa nishati safi ya kupikia ili kufikia azma ya Serikali ya kuhakikisha 80% watanzania wanaachana na matumizi ya kuni na mkaa ifikapo mwaka 2034

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »