Na Arodia PETER
WAZAZI wenye watoto wanaougua ugonjwa wa kifafa wameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kurudishia utaratibu wa Bima ya afya kwa watoto (Toto Afya Card) ili waweze kupata matibabu ya uhakika.
Walisema baada ya Serikali kusitisha utaratibu wa "Toto Afya Card" watoto wao wameacha kutumia dawa kutokana na gharama kubwa, hivyo kutishia uhai wao wa kuishi.
Ombi hilo kwa serikali lilitolewa na baadhi ya wazazi wenye watoto wanaishi na hali ya kifafa waliohudhuria kongamano lililiandaliwa Chama cha Wazazi Wenye watoto wenye kifafa Tanzania (UWAKITA) kwa kushirikiana na Idara ya Afya ya Akili Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Jumamosi Novemba 23 mwaka huu.
Mmoja wa wazazi hao, Glory Elihuruma Mrema mkazi wa Dar es Salaam alisema mtoto wake ameacha kwenda hospitali kuhudhuria kliniki na kupata dawa zaidi ya miezi 9 sasa kutokana na yeye kushindwa kumudu gharama hizo tangu bima ya watoto ilipositishwa na serikali.
Alisema gharama za matibabu kwa watoto wenye ukifafa zina gharama kubwa kwa mtu ambaye hana kipato cha kutosha, jambo ambalo linatishia uhai wa watoto hao pamoja na kuwasababishia wazazi msongo wa mawazo.
"Kwa mfano kidonge kimoja cha mil gram 500 kinauzwa shilingi 1500 kwa bei ya rejareja. Na kwa mujibu wa watabibu wetu, mtoto mmoja anapaswa kumeza vidonge vinne kila siku, yaani viwili asubuhi na viwili jioni, hapo bado dawa ya usingizi ambayo kidonge kimoja kinauzwa shilingi 500. Hivyo kwa siku moja mgonjwa wa kifafa anatumia Shilingi 6500.
"Kilio changu kwa Rais wetu, Samia Suluhu Hassan atuangalie kwa jicho la pekee, watoto wanaoishi na kifafa usalama wao ni dawa na chakula. Kama mtoto mwenye hali hiyo hajanywa dawa, ndani hapakaliki, wazazi tumebaki majumbani tunashindwa kufanya shughuli za kujitafutia kipato kwa sababu huwezi kumwacha huyu mtoto peke yake ndani." alisema Glory.
Mzazi mwingine, Avelia Said ambaye mtoto wake anaishi na kifafa kwa miaka 17 sasa, anasema kilio chake kwa serikali ni kupata matibabu ya uhakika kwa mtoto wake.
Alisema gharama za dawa kwa siku ni zaidi ya Shilingi 6000, na yeye hana kipato baada ya mumewe kufariki mwezi Agosti mwaka huu.
Anasema kwa sasa mtoto wake anaishi kwa kutegemea misaada ambapo mtu akimwonea huruma anamnunulia dawa za ziku tano au nusu mwezi, na zinapokwisha hali ya mtoto inazidi kuwa mbaya.
"Ombi langu kuu sisi wenye watoto wanaotegemea kuishi kwa dawa, serikali ituangalie kwa jicho la kipekee tupate hiyo bima ya watoto ili watibiwe kwa uhakika"alisisitiza Avelia.
Naye daktari bingwa wa magonjwa Afya ya akili wa hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt Kuganda Said alisema inahitajika elimu sahihi kwa jamii kuhusu ugonjwa wa kifafa kwamba dawa na wataalam wapo na unatibika.
Dkt.Kuganda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wazazi wa watoto wenye kifafa Tanzania (UWAKITA), alisema chama hicho kinasisitiza elimu juu ya ugonjwa huo na jamii ielewe kwamba wataalam wa wapo, vifaa vya uchunguzi vipo na ugonjwa wa kifafa unatibika, hivyo watu waache unyanyapaa kwani ni kikwazo kwenye tiba ya ugonjwa huo.
Kwa upande wake, Dkt. Nuruel Kitomary ambaye pia ni bingwa Afya na magonjwa ya akili wa Hospitali ya Taifa Muhimbili -Upanga Dar es Salaam, alisema zaidi ya watu milioni 50 duniani wanaishi na hali ya ukifafa; ambapo asilimia 80 wanatoka nchi zenye hali duni barani Afrika na Tanzania ikiwemo.
"Kati ya hao, watu milioni 10 wanaishi Afrika, na Tanzania inakadiriwa kuwa na watu 450, 000 mpaka 500,000 wanaoishi na hali ya ukifafa ambapo ni asilimia 3.7 tu ndiyo wapo kwenye matibabu.
"Hata hivyo hawa ni wale wenye usajili rasmi hospitalini, lakini kuna kundi kubwa nje ya hao ambao wamefichwa majumbani au wapo kwa waganga wa kienyeji, makanisani nakadhalika." alisema Dkt Kitomary.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa magonjwa yasiyoambukiza na afya ya akili kutoka Wizara ya Afya, Omary Ubuguyu alisema mkakati wa Serikali ni kuhakikisha vipimo na dawa ya msingi iitwayo phinobabitol inapatikana katika hospitali na vituo vya afya nchi nzima.
"Ingawa kuna dawa nyingine zaidi ya hiyo, lakini angalau hiyo ya msingi ambayo inasaidia kwa asilimia 70 wagonjwa wa kifafa inawasaidia.
Kuhusu bima ya afya, Dkt Ubuguyu alisema serikali ipo mbioni kukamilisha mpango wa afya kwa wote ambapo kila mtanzania atanufaika na huduma hiyo.
EmoticonEmoticon