BIL 36.596 ZA MRADI WA SEQUIP ZILIVYO INUFAISHA DODOMA KWENYE SEKTA YA ELIMU

July 24, 2025
Mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa maeneo ambayo yamepata fedha nyingi kupitia mradi wa kuimarisha ubora wa Elimu ya sekondari nchini SEQUIP ambapo umepokea zaidi ya Bilioni 36.596.

Fedha hizo ambazo zimetolewa na serikali zimetumika kujenga shule mpya 41 za Sekondari ambazo miongoni mwake ni pamoja na Shule 1 ya wasichana, Shule 1 ya kanda ya Wavulana, Shule za kata 36, Shule 1 ya Amali ya Mkoa, na Shule 2 za Amali za kata.

Hayo yamebainishwa na Afisa Elimu Mkoa wa Dodoma Mwl Vicent Kayombo ambapo amesema kuwa fedha hizo pia zimetumika kujenga Madarasa 77, Matundu ya Vyoo 119, Maabara 19, Mabweni 22, na Nyumba za Walimu 22.

Mwl Kayombo amesema kuwa mkoa wa Dodoma umejenga shule mpya ya wasichana Manchali kwa gharama ya Shilingi Bilioni 4.450 sambamba na ujenzi wa shule mpya ya Amali ya mkoa iliyojengwa katika kijiji cha Manchali wilayani Chamwino kwa gharama ya Shilingi Bilioni 1.6

Mwl Kayombo ameishukuru serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi katika mkoa wa Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ambazo zitapunguza umbali wa wanafunzi kwenda shuleni ikiwa ni pamoja na kuondokana na vishawishi njiani, na kuongeza muda wa wanafunzi kujisomea.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »