Na REA,
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeahidi kujenga mifumo ya nishati safi ya kupikia pamoja na jiko katika shule ya Sekondari ya mchanganyiko ya Ruhinda iliyopo Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera.
Ahadi hiyo imetolewa leo Novemba 7, 2024 na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy wakati wa muendelezo wa ziara ya viongozi mbalimbali wa Serikali waliambatana na Wabia hao wa Maendeleo ambao Serikali imekuwa ikishirikiana na kuwezesha upatikanaji wa nishati bora vijijini. Wabia hao ni Benki ya Dunia, Serikali ya Norway, Serikali ya Sweden, Umoja wa Ulaya, AFD na ADB.
Wakati wa ziara hiyo ambayo ililenga kutembelea miradi inayotekelezwa na Wakala huo, viongozi hao walitembelea Shule ya Sekondari ya Mchanganyiko ya Ruhinda ambapo katika risala yao, waliomba kupatiwa mfumo wa nishati safi ya kupikia.
“Tumeskia ombi lenu la kutamani kuwa na nishati safi ya kupikia hapa shuleni. Tutaenda kufanya tathmini na kuangalia nishati safi ipi itakayofaa zaidi. Tunaweza kuwa na mifumo hata miwili; mfumo wa gesi na mfumo wa majiko banifu ambayo yanatumia kuni kidogo na ni rafiki kwa mazingira.
Lakini pia kwa kuwa mifumo hii tunayotarajia kwenda kuifunga ni ya thamani na ya gharama kubwa. Pia tutawajengea na jengo la jiko zuri,” amesema Mkurugenzi Mkuu huyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali (mstaafu), Jacob Kingu amesema Wakala huo umekuwa ukiishi kwa vitendo maelekezo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk, Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni kinara wa nishati safi wa kupikia Afrika na Duniani kwa ujumla na kuongeza kuwa ujenzi wa mifumo ya kupikia katika shule hiyo ni kielelezo tosha cha utayari wa REA kupambana na nishati zisizo safi katika jamii.
“Tunajua shule ikibadilika kwa kutumia nishati safi ya kupikia hata wananchi wanaoizunguka shule hii pia watabadilika,” amesema Mwenyekiti Kingu.
Awali akisoma taarifa ya shule hiyo, Mkuu wa Shule hiyo, Ambruce Katorogo amesema kuwa shule hiyo inatumia Zaidi ya shilingi 800,000/= kila mwezi kwa ajili ya kununua kuni zinazotumika kupikia chakula cha wanafunzi shuleni hapo.
Awali Mkuu huyo wa shule pia aliishukuru Serikali kupitia REA kwa kuwezesha kufikisha nishati ya umeme katika shule hiyo ambapo imesaidia kuongeza usalama hasa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano kutoka REA, Bi. Martha Chassama ameendelea kuhamasisha wananchi kuendelea kutumia nishati safi ya kupikia na kusisitiza kuwa Wakala huo unaendelea na kampeni zake mbalimbali kuhamasisha wananchi wanajua madhara yatokanayo na nishati chafu ya kupikia.
Mwisho
EmoticonEmoticon