TANZANIA NA BENKI YA DUNIA WAJADILIANA UTEKELEZAJI MPANGO MAHSUSI WA NISHATI WA MISHENI 300

June 19, 2025


📌 *Mhandisi Mramba aeleza hatua zinazochukuliwa na Serikali kutekeleza Misheni 300*


📌 *Benki ya Dunia yapongeza*


📌 *Yaahidi kuendelea kuiunga mkono Tanzania*



Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felichesmi Mramba amekutana na Viongozi Waandamizi kutoka Benki ya Dunia ( WB) kwa lengo la kujadili hatua mbalimbali zilizofikiwa katika utekelezaji wa Mpango Mahsusi wa kuwafikishia  umeme Waafrika milioni 300 ifikapo 2030 ujulikanao kama Misheni 300.


Kikao hicho kimefanyika  katika Jiji la Cape Town nchini Afrika Kusini kando ya Mkutano wa Jukwaa la Nishati Afrika ambapo Tanzania inashiriki.


 Mhandisi Mramba ameeleza kuwa, katika Mpango huo uliosainiwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika uliofanyika mwezi Januari 2025, Tanzania kwa upande wake imeuweka Mpango huo kwenye mipango yake ya Serikali ili kutimiza malengo yaliyowekwa.


Amesema  kukamilika kwa Mpango huo kutaiwezesha Tanzania kuongeza upatikanaji umeme kutoka asilimia 78.4 ya sasa hadi asilmia 100 ifikapo mwaka 2030 na kuongeza matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia hadi kufikia asilimia 75 ifikapo 2030.


Kwa upande wao, Watendaji wa Benki ya Dunia, Bi.Yadviga Semikolenova, Meneja Mtendaji Ukanda wa  Kusini Mashariki mwa Afrika pamoja na Dkt. Rhonda  Antoine, Mtaalam Mwandamizi wa Nishati Ukanda wa Afrika wameipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua inazochukua ili kuhakikisha Mpango wa Misheni 300 unafanikiwa na hivyo kuwezesha wananchi kupata nishati ya uhakika. 

Aidha, Benki ya Dunia imeonyesha utayari wa kuendelea kuunga mkono juhudi  zinazofanywa na Tanzania  kuhakikisha inaendelea kuutekeleza mpango wa Misheni 300.


Katika kikao hicho, Mhandisi Mramba aliambatana na Mhandisi Innocent Luoga, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu pamoja na wataalam kutoka Wizara ya Nishati, TANESCO, REA, TPDC na EWURA

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »