DKT. BITEKO ASHIRIKI UAPISHO WA RAIS DUMA BOKO BOTSWANA

November 08, 2024
 


*Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati*
 
Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo Novemba 8, 2024 amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sherehe za uapisho wa Rais wa sita wa Botswana, Mhe. Gedion Duma Boko.

Katika uapisho huo uliofanyika katika Uwanja wa Taifa wa nchi hiyo, umeshuhudiwa na mamia ya wananchi wa Botswana na vitongoji vyake wakiwemo marais na viongozi wa wakuu kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Rais mteule wa Jamhuri ya Botswana ameapishwa rasmi kuwa Rais wa Sita wa nchi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano ambapo ameahidi kufanya kazi kwa kuzingatia misingi na sheria za nchi hiyo. Aidha amesema atatekeleza majukumu yake ya kazi akijielekeza katika kuleta maendeleo na Usatawi wa Nchi na Wananchi wake.
Akihutubia taifa kwa mara ya kwanza Rais Boko amesema anajivunia taifa lake la Botswana huku akiongeza kuwa matokeo ya ushindi na wake ni tukio la kihistoria kwake huku akiwataka wananchi wa Botswana kushikamana na kushirikiana katika kipindi kipya cha kisiasa ambacho amesema kinaongozwa na amani matumaini na kujijenga upya kijamii na kiuchumi.
“Tarehe 30 Oktoba tulithubutu kupima demokrasia, amani na utulivu wan chi hii na sasa najivunia kwamba tumeshinda mtihani kwa ushindi mkubwa” alisema na kuongeza kuwa matokeo haya yatapimwa usatawi wake katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Amesisitiza kuwa Botswana ni Jamhuri moja hakuna sababu ya kugawanyika bali umoja na mshikamano miongoni mwao na kusahau tofauti bali kuendelea kujenga kizazi kipya chenye matokeo makubwa zaidi ya sasa.

Awali wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi wa dini katika hafla hiyo, wameliombea taifa hilo kuwa na umoja na mshikamano huku wakihamasisha msamaha miongoni mwa viongozi na wananchi wote pamoja na kuomba utendaji uliotukuka kwa Baraza la Mawaziri ili waweze kufanya kazi kwa kutetea rasilimali za nchi hiyo. 
Sherehe hizo pia zimehudhuriwa na Rais wa Zimbabwe Mhe. Dkt. Emmerson Mnangagwa, Rais wa Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema, Rais wa Namibia, Mhe. Dkt. Namgolo Mbumba, Waziri Mkuu wa Eswatini, Mhe. Russell Mmiso Dlamini, Waziri Mkuu wa Afrika Kusini, Mhe. Ian Khama, Waziri Mkuu wa Msumbiji, Mhe. Adriano Afonso Maleiane, Jaji Mkuu wa Nchi hiyo, Spika wa Bunge na viongozi wengine waandamizi akiwemo Rais Mstaafu wa Botswana Mhe. Mokgweetsi Masisi.







Share this

Related Posts

Previous
Next Post »