*Ahoji matumizi ya Shilingi milioni 159 nje ya bajeti Ujenzi wa Kituo cha Afya Msimbati;
*Majibu ya Mkurugenzi wa Halmashauri, wataalam yatofautiana;
*Mkuu wa Mkoa asema suala hilo limewasilishwa TAKUKURU kwa Uchunguzi;
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amefanya ziara Mkoani Mtwara kukagua ujenzi wa miradi inayotekelezwa kwa fedha zinazotolewa na wawekezaji kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kama njia ya kurejesha rasilimali kwa wananchi (CSR).
Akikagua Kituo cha Afya Msimbati, Dkt. Biteko ameeleza kutoridhishwa na matumizi ya zaidi ya shilingi milioni 159 ikiwa ni zaidi ya fedha iliyokuwa imepangwa kutumika katika ujenzi wa Kituo hicho cha Afya ambacho awali kilikadiriwa kujengwa kwa gharama ya shilingi milioni 600 lakini gharama za ujenzi huo ziliongezeka hadi kufikia shilingi milioni 759 na hivyo kuibua maswali ambayo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mtwara, Abeid Kafunda amekiri kuwa hajui sababu za ongezeko la gharama hizo.
Akizungumzia hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala amesema uongozi wa Mkoa umekuwa ukifanya ziara kukagua miradi hiyo inayojengwa kutokana na utekelezaji maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara inakotoka gesi wanufaike na rasilimali hizo kupitia CSR.
Mheshimiwa Kanali Sawala amesema ufuatiliaji huo umebaini kuwa ujenzi wa mradi huo wa Kituo cha Afya Msimbati hauendani na thamani halisi ya fedha na hivyo kuwasilisha suala hilo katika Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Mtwara.
Akizungumza Sakata hilo, Dkt. Biteko amewataka watekelezaji wa miradi kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa kuzingatia kwamba miradi hiyo inakusudiwa kuwanufaisha Watanzania na sio vinginevyo.
“ Nimeelezwa kuwa jambo hili liko katika vyombo vya uchunguzi, nategemea watakuja na matokeo kulingana na kazi waliyoifanya, lakini wafanye kazi hii kwa haraka na kwa ubora, hapa ni mwanzo tu, kuna maeneo mengine miradi mikubwa zaidi itajengwa, tuhakikishe inatekelezwa kulingana na thamani halisi ya fedha” amesema Dkt. Biteko.
Baadaye Dkt. Biteko amefanya ukaguzi wa majengo ya Kituo cha Afya Msimbati ambacho ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 98.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Dkt. Biteko amekagua ujenzi wa Kituo cha Polisi Kata ya Msimbati ambacho kimekamilika na maombi ikiwa ni ujenzi wa Uzio, samani, mifumo wa ya TEHAMA na, maji nyumba ya makazi ya Mkuu wa Kituo.
Wakazi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara wamekuwa na kilio cha muda mrefu wakiomba huduma za maendeleo kutokana rasilimali ya gesi kuchimbwa katika mikoa hiyo suala lililoisukuma Serikali kuagiza TPDC kutoa fedha kupitia CSR ili iweze kunufaisha wananchi kama inavyotokea katika maeneo mengine ya Nchi.
Kufuatia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko alielekeza kujengwa kwa kituo cha Afya katika eneo la Msimbati, Kituo cha Polisi pamoja na Uwekaji wa taa za Barabarani katika eneo hilo.
EmoticonEmoticon