WAZIRI CHANA KUZINDUA ALAMA YA ASALI YA TANZANIA MKOANI TABORA

October 03, 2024

 

Sehemu ya wajasiriamali wanaozalisha asali na mazao mengine yanayotokana na asali wakiwa katika maonesho ya asali katika Chuo cha Nyuki mkoani Tabora ambapo kesho Oktoba 4,2024 kutafanyika uzinduzi wa alama ya asali ya Tanzania.

Na Mwandishi Wetu Michuzi TV ,Tabora
WAZIRI wa Maliasili na Utalii mheshimiwa Balozi Dk.Pindi Chana kesho Oktoba 4,2024 atazindua alama ya asali ya Tanzania katika chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki mkoani Tabora yenye lengo la kuitangaza asali ya Tanzania katika soko la kimataifa.

Akiongea na waandishi wa habari mkoani Tabora, Mwenyekiti ya Kamati ya kuandaa uzinduzi wa alama hiyo, Kamishina Msaidizi Mwandamizi kutoka Wakala wa Misitu Tanzania(TFS) Hussen Msuya amesema licha ya kuitangaza nchi, alama hiyo pia ni kithibitisho kingine cha ubora wa asali inayozalishwa nchini Tanzania na kuuzwa katika masoko ya kimataifa.

Amesema uzalishaji asali nchini Tanzania umekuwa na tija kubwa katika kukuza uchumi wa wafugaji nyuki, wafanyabiashara wa mazao yanayotokana na mnyororo wa thamani wa asali na Serikali kwa ujumla ambapo kwa mwaka jana, zao hilo pekee liliingiza takriban dola milioni 19.

“Alama hii itazidi kukuza soko la asali ya Tanzania kimataifa,”

“Tayari kwa sasa tunajivunia soko kubwa katika nchi mbalimbali za Ulaya ikiwemo Ujerumani na Marekani kwa upande wa bara la Amerika na nchi nyingine mbalimbali duniani,”

“Hivyo, uzinduzi wa alama hii utazidi kuwanufaisha wazalishaji asali na Nta, ambapo takriban watu milioni mbili wanashiriki katika mnyororo wa thamani wa zao la asali linalotegemea zaidi ya wafugaji nyuki laki nane,” amesema.

Uzinduzi wa alama hii, kwa mujibu wa Msuya, ni sehemu ya maandalizi ya nchi kimkakati katika utambuzi wa asali ya Tanzania katika soko la kimataifa, ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji wa maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani ( Apimondia) mwaka 2027 itakayoshirikisha wafugaji nyuki kutoka nchi mbalimbali duniani.

Mmoja wa washiriki Simon Majeni kutoka kampuni ya Salbena Honey amesema hii ni fursa kubwa kwa ukuaji wa soko la asali kufutia jitihada kubwa zinazofanywa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuipa thamani asali ya Tanzania na kukuza uchumi wa nchi, wafugaji na wafanyabiashara wa mazao ya asali kwa ujumla.

Kupitia alama itakayozinduliwa, amewataka wafanyabiashara kuongeza thamani katika vifungashio na kuitangaza vizuri ili izidi kukamata soko la kimataifa.

Amesema kupitia mradi wa kuongeza mnyororo wa thamani ufugaji Nyuki (BEVAC), wajasiliamali kupitia wadau mbalimbali wa maendeleo wamekuwa wakipewa mafunzo mbalimbali ya ufugaji bora na urinaji wa asali kwa ajili ya soko la kimataifa.

" Tunawashukuru sana wadau kwa hatua hii itakayoleta mapinduzi katika zao la asali na mazao engine yanayopatikana katika mnyororo wake wa thamani ,"amesema.

Uzinduzi huu umefadhiliwa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya na kutekelezwa kwa pamoja na Shirika la Maendeleo la Ubelgiji (Enabel) na Kituo cha Biashara cha Kimataifa (ITC) ambapo alama hii itasimamiwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade).


Sehemu ya wajasiriamali wanaozalisha asali na mazao mengine yanayotokana na asali wakiwa katika maonesho ya asali katika Chuo cha Nyuki mkoani Tabora ambapo kesho Oktoba 4,2024 kutafanyika uzinduzi wa alama ya asali ya Tanzania.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »