Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) akijibu swali, bungeni jijini Dodoma la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Shally Raymond aliyetaka kufahamu ni lini kampuni za simu zitalazimishwa kutoa elimu kwa wananchi kabla ya kutoa mikopo, kwa kuwa kampuni za simu ndizo zinazoongoza kutoa mikopo kwa haraka bila kujaza fomu au chochote ambapo vijana na wajasiriamali wengi wakiwemo wakina mama huvutiwa nayo.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha - Dodoma)
Na. Joseph Mahumi, WF, Dodoma.
SERIKALI imesema inafuatilia kwa karibu mwenendo wa utoaji wa mikopo kwa njia ya kidigitali iliyoidhinishwa na kwamba itakapobainika kuwa kuna ukiukwaji wa matakwa ya leseni ya utoaji wa mikopo hiyo hatua stahiki zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwafutia leseni watoa huduma husika.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Shally Raymond aliyetaka kufahamu wakati ambapo kampuni za simu zitalazimishwa kutoa elimu kwa wananchi kabla ya kutoa mikopo, kwa kuwa kampuni za simu ndizo zinazoongoza kutoa mikopo kwa haraka bila kujaza fomu au chochote ambapo vijana na wajasiriamali wengi wakiwemo wakina mama huvutiwa nayo.
Dkt. Nchemba alisema, kwa mujibu wa sheria za fedha zinazosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania, hakuna kampuni ya simu iliyopewa leseni ya kutoa mikopo kwa wananchi kwa kuwa ili kampuni, taasisi au mtu binafsi aweze kutoa mikopo kwa wananchi anapaswa kuwa na leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania na kukidhi matakwa ya Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha (The Banking and Financial Institutions Act, 2006) na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha (Microfinance Act, 2018).
Aliongeza kuwa, Kampuni za simu zinazotoa huduma za fedha zimepewa leseni ya kutoa huduma za mifumo ya malipo kulingana na matwaka ya sheria ya Mifumo ya Malipo ya Taifa ya mwaka 2015 (The National Payment Systems Act, 2015) pamoja na kanuni zake. Kampuni hizo zipo sita (6) ambazo ni: M-Pesa Limited, Honora Tanzania Mobile Solution Limited (Tigopesa), Airtel Money Tanzania Limited (Airtel Money), Viettel Ecommerce Limited (Halopesa), TTCL Pesa Limited (T-Pesa), na Azam Pesa Tanzania Limited (AzamPesa).
“Mikopo inayotolewa kwa wananchi kupitia simu za kiganjani hutolewa kwa ushirikiano kati ya taasisi zilizopewa leseni ya kutoa mikopo na kampuni za simu zilizopewa leseni ya mifumo ya malipo, ushirikiano huu unaainisha majukumu ya kila mtoa huduma ambapo taasisi zinazotoa mikopo hutoa mikopo hiyo kulingana na sheria na kanuni za leseni za utoaji mikopo huku kampuni za simu zikitoa mifumo, wateja na mwenendo wao wa kutumia huduma za kifedha” alisema Dkt. Nchemba.
Aidha, Dkt. Nchemba aliongeza kuwa mikopo yote hutolewa kupitia benki na watoa huduma ndogo za fedha ambapo inawafikia wananchi wote wenye uhitaji na wenye kutumia huduma za kifedha kupitia simu za mkononi kwa kutumia mifumo ya malipo ya kampuni za simu ambayo wateja wao wapo nchi nzima.
Alisema kuwa hatua hiyo imewasaidia wananchi kupata mikopo bila uhitaji wa kuwa na akaunti ya benki wala dhamana ya mkopo husika.
Dkt. Nchemba alisema kuwa, kwa mujibu wa Kanuni za Kumlinda Mtumiaji wa Huduma za Fedha za mwaka 2019, watoa huduma wote wa fedha wanaosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania wanatakiwa kutoa elimu ya fedha kwa wateja wao juu ya huduma zao wanazotoa, ikiwemo elimu ya mikopo ambapo kanuni hizo zinawataka kutoa mikopo baada ya mkopaji kuridhia masharti ya mkopo husika.
Alisema kuwa pamoja na Benki Kuu kuwahimiza watoa huduma za fedha kutoa elimu kwa wateja wao, Benki Kuu ya Tanzania katika nyakati tofauti imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi juu ya huduma za fedha na kuwataka kutojihusisha na huduma za kifedha kutoka kwa watoa huduma wasio na leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania.
“Mikopo iliyopata umaarufu wa kuitwa “Kausha Damu” hutolewa na taasisi ambazo hazina leseni ya Benki Kuu ya Tanzania, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imechukua hatua mbalimbali za kuzuia mikopo hii ikiwa ni pamoja na kuzitaka kampuni za simu kuhakikisha mifumo yao haitumiki katika shughuli zozote zinazohusiana na mikopo hiyo pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waepukane na kuchukua mikopo hiyo. Vile vile, Serikali inaendelea kuwafuatilia wahusika ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi ya wanaokiuka taratibu zilizowekwa” alisema Dkt. Nchemba.
Dkt. Nchemba alitoa rai kwa Benki Kuu ya Tanzania kuimarisha usimamizi wa sekta ya fedha hususan watoa huduma ndogo za fedha pamoja na watoa huduma za mifumo ya malipo kuhakikisha wanazingatia matakwa ya Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Sheria ya Mifumo ya Malipo ya mwaka 2015 pamoja na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2015.
Aidha aliwasihi wanachi wapate huduma za fedha kwa watoa huduma rasmi wanaosiimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania ili kuepuka kutumia huduma za fedha kutoka kwa watoa huduma wasio rasmi na masharti magumu ikiwemo riba kubwa.
EmoticonEmoticon