DKT KARATA AIPONGEZA SERIKALI KWA KUWEKA MPANGO MZURI WA UTOAJI WA DAWA ZA KUPUNGUZA MAKALI KWA WARAIBU WA DAWA ZA KULEVYA

January 14, 2024


Na Mwandishi Wetu,Tanga

DAKTARI wa Afya ya Akili katika kituo cha Methadone (MAT) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga –Bombo Dkt Wallace Karata ameipongeza Serikali kuweka mpango mzuri wa utoaji wa dawa za kupunguza makali kwa waraibu wa dawa za kulevya na matokeo yake yamekuwa mazuri.

Matokeo hayo yameweza kuleta mabadiliko na wapo ambao wamekamilisha matibabu yao wapatao 28 na wanaendelea vizuri katika jamii kutokana ikiwemo kubadilika na kuachana na matumizi.

Dkt Karata aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na mtandao huu ambapo alisema mpango huo wa Serikali kupitia Wizara ya Afya washirikiana na wadau wa Maendeleo umesaidia kuwezesha kupatikana vifaa kazi ambavyo vitawasaidia waweza kujikwamua kiuchumi.

Alisema katika mpango huo watakuwa na mashine za kufyetulia Tofali,Mashine za kuosha Magari (Car wash),Mashine za Salooni,Mashine za Kushonea nguo na watakuwa wanawaandaa vijana na shughuli za uzalishaji mali katika Jiji la Tanga baada ya kupata nafuu.

“Jambo hili ni hatua kubwa sana na yakupongezwa kwani changamoto iliyopo kwenye jamii ni ukosefu wa shughuli za kufanya baada ya kupata nafuu lakini mpango huo utakuwa chachu yao kushiriki shughuli za kiuchumi na hatimaye kupata maendeleo”Alisema

“Katika kituo chetu hapa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo tunatoa huduma kwa waraibu wa dawa za kulevya aina ya hereion na mchanganyiko wa dawa mbalimbali ikiwemo Ugoro,Pombe,Mirungi na mwamko upo kwenye jamii kutokana na kufanya kazi na asasi za kiraia ambao wamekuwa wakiwaibua watumiaji wa dawa za kulevya kwenye mitaa mbalimbali”Alisema

Dkt Karata alisema Asasi hizo zimekuwa zikiwaandaa na kuwapelekea ili kuweza kuendelea nao kwenye tiba ambayo ni kuwasaidia kuwaondolea maamivu ya arosto kwa kutumia dawa ya methadone na kuweza kuwapa tiba za kisaikolojia.

“Kwa sasa kila siku tunasajili waraibu wawili mpaka watatu kwa siku ambapo kwa wiki idadi inafikia 12 mpaka 13 hii inatokana na uwepo wa Asasi za Kiraia ambazo zimekuwa zikiwaibua waraibu wa dawa za kulevya kutoka kwenye vijiwe na fukwe na maeneo wanayopatikana wakiwa wanafanya matumizi ya dawa hizo”Alisema

Hata hivyo Dkt Karata alitoa wito kwa jamii kupeleka elimu kinga kwa wale ambao hawajaanza kuingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya ili kuweza kudhibiti matumizi mapya

“Lakini pia niwaombe viongozi wa dini wakiwemo Mashehe, wachungaji na Maaskofu wachukulie uraibu kama ugonjwa tena sugu wa akili na waone huo ni mpango mbaya wa shetani kuharibu vizazi vyetu hivyo watumie nafasi zao kuhakikisha wanakemea “Alisema

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »