OPERESHENI MAALUM YA DCEA YABAINI KIWANDA CHA KUTENGENEZA BISKUTI ZENYE BANGI JIJINI DAR

November 08, 2023

 *Pia wanasa kilo 423 za bangi, yatoa tahadhari ya ulaji vyakula kwa wanafunzi


Na Said Mwishehe, Michuzi TV

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imekamata kilo 423.54 za bangi iliyosindikwa maarufu kama Skanka huku pia kubaini uwepo wa kiwanda cha kutengeneza biskuti zilizochanganywa na bangi katika eneo la Kawe jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo Novemba 8, 2023 jijini Dar es Salaam Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema wamekamata Skanka baada ya kufanyika operesheni maalum zilizofanyika kwenye mipaka na fukwe za Bahari ya Hindi.

Amefafanua kilo 158.54 zilikamatwa eneo la Kigamboni na Kawe jijini Dar es Salaam zikiwa zimehifadhiwa ndani ya mabegi ya nguo tayari kwa kusafirishwa , kilo 265 zilikamatwa katika matukio tofauti mikoa ya nyanda za juu Kusini zikiwa zimefichwa ndani ya magari kwa kuchanganywa na bidhaa nyingine ikiwemo maboksi yenye matunda aina ya Apples zikisafirishwa kuelekea jijini Dar es Salaam.

Pia amesema Mamlaka hiyo imekata watu wanaojihusisha na utengenezaji wa biskuti kwa kuchanganya na Skanka katika eneo la Kawe huku akifafanua katika tukio hilo watuhumiwa walikutwa wakiendelea na uzalishaji wa biskuti hizo kwa kutumia mtambo mdogo wa kusaga skanka na vifaa vya kutengeneza biskuti za bangi.

Akifafanua zaidi mbele ya waandishi wa habari , amesema Mamlaka imebaini maeneo yanayotumika kama masoko ya kusambazia na kuuza Skanka kwenye fukwe ya Bahari ha Hindi .

"Kutokana na operesheni hizo meongeza katika operesheni hizo watu 16 wamekamatwa ambapo kati yao sita wamefikishwa mahakamani na 10 watafikishwa baada ya taratibu za kisheria kukamilika."

Akifafanua kuhusu Skanka( Skunk) amesema ni jina la mtaani linaloitambulisha aina ya bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu ikilinganishwa na bangi ya kawaida.

Ameongeza dawa hiyo ya kulevya hutokana na kilimo cha bangi mseto ambapo asilimia 75 ni bangi aina ya Sativa na asilimia 25 ni bangi aina ya Indica."Kiwango cha sumu kilichopo kwenye sanka ni zaidi ya asilimia 45 ukilinganisha na bangi ya kawaida ambayo kiwango chake cha sumu ni kati ya asilimia 3 mpaka 10.

"Hivyo Skanka ina madhara makubwa zaidi kwa mtumiaji ikiwemo kuamsha na kuzidisha magonjwa ya afya ya akili kwa haraka.Imebainika kuwa watu wasiowaaminifu huchanganya sanka kwenye vyakula kama vile biskuti, keki, jamu , sharubati , tomato souce pia kwenye sigara na shisha.

" Lengo la kufanya hivyo ni kurahisisha uuzwaji wa dawa hizo kwa kuficha na kuongeza idadi ya watumiaji wa dawa za kulevya hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya vyakula hivyo hupendwa na watoto, "amesema.

Lyimo amesema wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo wanapaswa kuwa makini na vyakula hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya vyakula hivyo hupendwa na watoto.

Pamoja na hayo amesema Mamlaka hiyo inaendelea kufanya operesheni dhidi ya wasafirishaji na wazalishaji wa dawa za kulevya katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha dawa za kulevya haziendelei kuwepo nchini.

" Tunawaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za wahalifu wa dawa za kulevya kwa kupiga namba ya bure ya 119 ambapo taarifa zitapokelewa kwa usiri mkubwa na kufanyiwa kazi."

Hata hivyo alipoulizwa Mamlaka inampango gani wa kuchukua hatua kwa baadhi ya wauza shisha ambao wanachanganya na bangi, amejibu kuwa kwa sasa wapo katika mchakato wa kuwepo kwa sheria hivyo itakapokamilika Mamlaka itatoa taarifa kuhusu shisha.

Alipoulizwa ni hatua gani zinachukuliwa na Mamlaka hiyo kudhibiti uzalishaji wa biskuti zinazochanganywa na bangi pamoja na aina nyingine ya vyakula, amejibu wameendelea kuchukua hatua ikiwa pamoja na kuvunja mtandao wa wazalishaji wa biskuti hizo akitolea mfano wote waliokuwa wanahusika na kiwanda kilichopo Kawe wamekamatwa na kesi iko mahakamani na wengine wamefungwa.

Amesisitiza Mamlaka imeendelea na mapambano dhidi ya dawa za kulevya na hivyo kusababisha dawa za kulevya kupungua nchini na matokeo yake waraibu wa dawa hizo wanalazimika kutumia dawa mbadala pamoja na dawa za Waraibu

Aidha amesema kutokana na kufanyika kwa operesheni ya kutokomeza dawa za kulevya nchini hivi sasa wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa hizo kuingiza bangi kutoka nchi nyingine lakini Mamlaka imeimarisha ulinzi mipakani ili kuhakikisha hakuna dawa za kulevya zinazoingia nchini.






Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo
 

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »