WAZIRI MKENDA AONGOZA TEAM YA TANZANIA MKUTANO WA ACAT

October 31, 2023

Na: Calvin Gwabara – Nairobi.

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda ameongoza timu
ya Serikali ya Tanzania kwenye mkutano mkubwa wa Teknolojia za Kilimo
Afrika (ACAT) ulioanza leo jumatatu nchini Kenya.


Mara baada ya kufika kwenye viwanja vya mkutano huo mkubwa
akiongozana na Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Balozi Dkt. Benard
Yohana Kibesse pamoja na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na
Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amos Nungu na watumishi wengine wa
Serikali ametembelea maonesho mbalimbali ya Teknolojia za kilimo
zinazooneshwa nje ya mkutano huo.


“Nimeona maonesho ambayo kimsingi ni kuhusu jinsi Sayansi na
Teknolojia inavyoweza kuleta mabadiliko chanya kwenye kilimo pamoja na
ukweli huu tumeona pia umuhimu wa kuzingatia usalama na afya kwenye
mabadiliko haya na pia kuchukua tahadhari tusipoteze umiliki wa yale
tunayogundua, hasa mbegu bora, ili tusiingie kwenye utegemezi
utakaotudhoofisha” alisema Prof. Mkenda.


Tanzania kupitia wizara yake ya Elimu Sayansi na Teknolojia na taasisi
zilizo chini yake imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika kuhakikisha nchi
inawezesha wabunifu kupitia Programu zake mbalimbali ikimwemo.


Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi Teknolojia na Ubunifu ( MAKISATU)
ambayo yanafanyika kila mwaka kwa kuhusisha wabunifu mbalimbali
kuanzia kwenye jamii, Shule za Msingi na Sekondari, Vyuo Vya kati, Vikuu
pamoja na Taasisi za Utafiti na kuwapatia washindi fedha na mahitaji
mengine ili kuwezesha kukuza bunifu zao na kuzibiasharisha.


Mkutano huo utazinduliwa siku ya jumanne ya tarehe 31/10/2023 na Rais
wa Jamhuri ya watu wa Kenya Mhe. Dkt. William Samoei Ruto na
kuhudhiriwa na mamia ya wadau wa kilimo kutoka Afrika na Dunia nzima.


Aidha Mkutano huo wa (ACAT) umeandaliwa na Serikali ya Kenya kupitia
Wizara yake ya Kilimo na Maendeleo ya Ufugaji kwa kushirikiana na
Taasisi ya Teknolojia za Kilimo Afrika (AATF)








Share this

Related Posts

Previous
Next Post »